Kuimarika kwa Sekta Binafsi kutasaidia ajira kwa Vijana – Waziri Jaffo

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jaffo, amesema kuimarika kwa sekta binafsi kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya juu nchini.

Dk. Jaffo aliyasema hayo leo, Julai 6, 2024, wakati wa Siku Maalum ya China iliyoambatana na Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kitaifa (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam. Alitoa wito kwa wawekezaji kutoka China na mataifa mengine kuwekeza nchini ili kukuza uchumi na kutoa ajira kwa vijana.

“Taarifa inaonesha kwamba tunasafirisha bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.3, lakini tunaingiza bidhaa kutoka China zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 3.5,” alisema Dk. Jaffo.

Alisisitiza kuwa uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China umeleta faida kubwa kwa nchi hizo, hasa katika uchumi kwa kusafirisha bidhaa. Aliongeza kuwa uhusiano huo pia umewezesha ujenzi wa viwanda vya Kichina hapa nchini, kutoa ajira, na kujenga miundombinu kupitia kazi za ukandarasi.

Dk. Jaffo alibainisha kuwa kampuni 100 kutoka China zimeweza kushiriki katika maonesho hayo ya 48 ya biashara ya kimataifa, jambo linaloonyesha mvuto wa uwekezaji nchini. Alisema serikali imejipanga kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wawekezaji wanapata fursa ya kuwekeza nchini.

Alihimiza kuendelea kwa ushirikiano huo na uwekezaji ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana. “Vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu na serikali haiwezi kuajiri vijana wote,” alisema Dk. Jaffo, akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kutoa ajira.

Kwa kumalizia, alikaribisha wawekezaji kuwekeza nchini ili kusaidia katika kupunguza tatizo la ajira na kukuza uchumi wa taifa.

Related Posts