YANGA imetoa taarifa mpya juu ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano na kwamba sasa itaanza tena palepale ilipojiandaa kuchukua mataji nane ndani ya misimu mitatu ambapo mastaa wote wapya waliosajiliwa na wale walioongezewa mikataba watakuwa hadharani kuanzia keshokutwa Jumatatu.
Taarifa mpya kutoka Yanga inasema kikosi hicho sasa kitarudi rasmi kambini kuanza mazoezi, Julai 8 palepale Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambako wamekuwa wakijiandaa hapo kwa misimu mitatu.
Ikitokea hapo Yanga imechukua mataji nane ya ndani yakiwemo matatu ya Ligi Kuu Bara, matatu ya Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao za Jamii mbili ikiikosa moja tu msimu uliopita iliyochukuliwa na Simba.
Awali hesabu za Yanga zilikuwa mbili kwamba ikajiandae kati ya Russia au Afrika Kusini walikopata mialiko mbalimbali na wenyeji wao lakini sasa mambo yakabadilishwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema siku hiyo wachezaji wote wakiwemo wapya waliosajiliwa na wale waliosalia watatakiwa kufika Avic Town kuanza maandalizi yao na benchi lao la ufundi chini ya Miguel Gamond.
“Tutaanza maandalizi yetu hapo Avic hiyo ndio taarifa rasmi, kila mchezaji aliyesajiliwa kwa msimu ujao atakuwepo pamoja na wale wa zamani, tuna majukumu makubwa msimu ujao wa kutetea mataji yetu na tunahitaji kufika mbali kwenye mashindano ya Afrika,” alisema Kamwe.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa timu hiyo bado wanasita kuitoa timu nje ya Tanzania ikihofia muda mfupi uliosalia kabla ya kuanza msimu wa mashindano.
Yanga itakuwa na mchezo wa wiki ya Mwananchi Agosti 4 ikiwa zimesalia siku 27 pekee mpaka siku hiyo kubwa kwa klabu hiyo ambazo ni chache kwa maandalizi ya msimu mpya.
Baada ya kilele cha wiki ya Mwananchi Yanga itaanza kufikiria ratiba ya mechi za Ngao ya Jamii zitakazoanza Agosti 8-11 ambapo mabingwa hao watafungua pazia kwa kukutana na watani wao Simba. Timu nyingine shiriki ni Azam FC na Coastal Union.
Hadi sasa sasa Yanga imeshamtambulisha Clatous Chama kutoka Simba, huku ikielezwa imeshamalizana na Jean Baleke, Prince Dube, Boka na kuwasainisha upya kina Farid Musa, Djigui Diarra, Abuutwalib Mshery, Bakar Mwamnyeto na Nickson Kibabage.