Dodoma. Uzalishaji wa zabibu nchini unatarajiwa kupungua mwaka huu, kutokana athari za mabadiliko ya tabia nchi zilizosababisha msimu mrefu wa mvua.
Akizungumza leo Jumamosi, Julai 6, mwaka 2024 na Mwananchi, Mwenyekiti wa Wakulima wa Zabibu mkoani Dodoma, David Mwaka amesema kuwa mvua mwaka huu ilinyesha hadi Aprili, hivyo joto la Mei halikutosheleza zabibu kuzaa vizuri.
“Ukienda shambani unaweza kushangaa zabibu ukiiona ni tofauti kabisa yaani mimi naona kuwa imepungua kwa nusu ya mwaka jana … Pia mvua ilileta sana magonjwa katika zabibu na hivyo kusababisha zabibu kuharibika kwa kuwa maji yalituama katika baadhi ya mashamba,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Kusindika Mvinyo cha Alko Vantages, Archard Keto amesema lengo la kiwanda hicho ni kuongeza uzalishaji wa mvinyo kutoka lita milioni 2.2 hadi lita milioni tano upatikanaji wa zabibu ni muhimu.
Amesema katika mwaka huu, kilimo cha zabibu kimeathirika sana na hali ya hewa na hivyo kutotegemea zabibu nyingi ulikilinganisha na mwaka jana ambapo baadhi yake ziliozea shambani.
Amesema ushirikiano kati yao na wakulima katika kutoa mikopo na elimu juu ya kuboresha kilimo hicho, ni muhimu ili wasiathirike na hali ya hewa na hivyo kusababisha upungufu wa malighafi.
“Ndio maana tunataka kusaidia suala la visima ili tatizo la ukame lisiweze kuwa kikwazo cha kuongeza wingi wa zababu,” amesema.
Amesema wakulima wamekuwa nguzo kubwa katika kiwanda hicho kuhakikisha wawapatia zabibu zenye ubora kupitia vikundi vyao na kwa sasa Alko Vintages inafanyakazi na wakulima 1,200 wa Dodoma.
Kwa mujibu wa Kato, kwa mwaka 2023 pekee kampuni ilinunua zabibu zenye thamani ya Sh5 bilioni ikiwa ni miongoni mwa viwanda 15 vya kusindika zabibu vilivyopo mkoani hapa.
Akizindua bidhaa mpya za mvinyo zilizobuniwa na kiwanda cha Alko Vintages chini ya utaalamu kutoka Afrika Kusini jana usiku, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Serikali itaendelea kulea viwanda na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Amesema sasa hivi mvinyo wa Tanzania unakidhi viwango vya kimataifa na hivyo unywaji wa mvinyo kutoka nje ya nchi umezidi kupungua kwa watu kunywa bidhaa hiyo inayotengenezwa nchini.
Profesa Mkumbo ametoa wito kwa wawekezaji kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwa jambo la muhimu ni kuwasaidia wakulima ili waongeze uzalishaji.