Dar ea Salaaam. Siku saba ya baada ya mjumbe wa zamani wa Kamati Kuu Chadema, Mchungaji Peter Msigwa kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makala amesema wapo wanasiasa wengine watakaohamia chama hicho tawala.
Juni 30, 2024 Mchungaji Msigwa ambaye ni mwenyekiti wa zamani kanda ya Nyasa, alijiunga na CCM na kupokelewa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam kikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.
Akihutubia wanachama na viongozi wa CCM mkoani Dar es Salaam, katika kikao cha ndani kilichofanyika jijini hapa, Makalla amewataka wana-CCM kujiandaa na bomu jingine, akiwa na maana ya kuwapokea wageni kutoka vyama vya upinzani watakaojiunga na chama hicho tawala.
“Bado tutapiga bomu mochwari, tutaleta watu wengi, kaeni mkao wa kula wapo wengi watakaokuja ndani ya CCM, ” amesema Makalla huku akishangiliwa kwa kupigiwa makofi na wanachama wa chama hicho.
Amesema Msigwa alikuwa kigogo mzito ndani ya Chadema akihudumu nafasi mbalimbali za ujumbe wa kamati kuu na uenyekiti wa kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa na Njombe, lakini ameamua kujiunga na CCM.
Makalla amesema kuanzia kesho Jumapili Julai 7, 2024 makada wapya wa CCM, Upendo Peneza na Mchungaji Msigwa wataonekana majukwaani kueleza sababu ya kuhama Chadema.
Licha kwamba Makalla hajaweza wazi lakini taarifa za uhakika ambazo Mwananchi Digital linazo, baadhi ya wabunge 19 maarufu ‘Covid-19’ watajiunga na CCM.
Baadhi ya wabunge hao 19 akiwemo Halima Mdee, tayari wamekwisha kuanza maandalizi ya kuweka sawa majimbo ambayo watawania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao 2025.