Mipango wa mazishi ya mvulana mwenye umri wa miaka 12 aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya kupinga muswada wa fedha nchini Kenya imeingia doa baada ya polisi kutokomea na mwili wa marehemu. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Mama yake marehemu Kennedy Onyango alikuwa amesafiri kutoka Nairobi hadi eneo la Mbita, Kaunti ya Homabay nchini humo jana Ijumaa lengo la kwenda kuusitiri mwili wa mwanaye lakini kundi la polisi lilidaiwa kuuchukua mwili huo kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Katika video iliyochapishwa na mchekeshaji, Eric Omondi leo Jumamosi, mama huyo ameomba serikali kumsaidia kurejesha mwili wa mwanawe ili aweze kupata nafasi ya kumzika.
Jana nilisafiri na mwili wa mtoto wangu kwa lengo la kuja kuuzika. Mtu akifariki duniani ukimzika ndio unajua umemsitiri na hilo ndio kaburi lake. Kufika huku Mbita tukanyang’anywa mtoto na maaskari. Hadi sasa sijaona mtoto wangu, sijamuona mtoto wangu. Serikali nisaidie nizike mtoto wangu,” mama’ke Kennedy alilalamika kabla ya kuangua kilio.
Waombolezaji wengine waliokuwa na mama marehemu walisikika wakilalamika pia na kushangaa mwili wa mtoto umefanya nini.
“Nimenyang’anywa mtoto wangu! Kwa nini nimenyang’anywa mtoto wangu? Kwani hii Kenya tuko Kenya gani? Mpaka unanyang’anywa mtoto wako. Yaani naomboleza mtoto wangu, mwingine yupo na roho ya kuninyang’anya. Mungu wangu. Naomba mtoto wangu,” mama’ke Kennedy aliendelea kulia.
Akielezea hali hiyo, mchekeshaji Eric Omondi ambaye alikuwa ameungana na mama’ke kwenye mazishi hayo, alisema walipata kizuizi cha barabarani walipokuwa wakisafiri kwenda kumzika mvulana huyo kabla ya mwili kudaiwa kuchukuliwa.
“Kwa hivyo, tulifika Homabay kumzika Kennedy mwenye umri wa miaka 12 na kabla ya kufika nyumbani tulikuta kizuizi cha barabarani cha polisi. Wakamchukua yule kijana. Yeyote anayehusika naomba mruhusu mwanamke huyu aomboleze kwa amani mruhusu amzike mwanae. Ameteseka vya kutosha,” Eric alisema.
Mtoto huyo aliyefariki baada ya kudaiwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ambayo yalishuhudiwa hivi majuzi nchini humo alitambuliwa kwa jina la Kennedy Onyango.
Picha za majeraha ya risasi mgongoni ziliwatia hofu Wakenya kwenye mitandao ya kijamii na walitaka haki itendeke kwa mvulana huyo.
Zaidi ya majeraha manane ya risasi yalionyesha wakati polisi wakipambana na waandamanaji.