RAFIKI zetu Wachina sio watu wanafiki sana. Wana bidhaa zao huwa wanatengeneza kwa ajili ya Afrika, halafu wana bidhaa wanatengeneza kwa ajili ya Wazungu wa mataifa yaliyoendelea. Bidhaa zenye ubora zaidi.
Watoto wetu wanaozaliwa Ulaya wakati mwingine wanajikuta kama bidhaa tu. Kuna bidhaa zenye ubora zinabaki kwao, halafu kuna bidhaa ambazo wanaleta Afrika. Mara chache sana wamekubali kutuachia bidhaa bora zije Afrika.
Mfano ni hawa watoto wawili. Inaki Williams na mdogo wake Nico Williams. Umewatazama wote vizuri? Wapo pale Athletic Bilbao, Hispania. Baba mmoja, mama mmoja. Inaki amezaliwa Bilbao wakati mdogo wake amezaliwa mji wa kando, Pamplona.
Inaki ameichezea Hispania mechi moja tu, lakini ni mkongwe wa Bilbao. Mshambuliaji wao punda. Mpambanaji. Hata hivyo sidhani kama alikuwa mzuri kiasi hicho. Mwenyewe amekimbilia zake Afrika kucheza Ghana – taifa ambalo ni asili yake na mdogo wake, Nico.
Inaki ana miaka 30 tu. Hakuwa mzuri hivyo kushindana na kina Alvaro Morata pale mbele. Wazungu wakaona isiwe shida. Na yeye mwenyewe akaona isiwe shida. Akaamua kujifanya mzalendo kuchezea taifa la asili yake, Ghana.
Ndiyo, alijifanya mzalendo na hakuwa mzalendo halisi. Kama angekuwa mzalendo halisi kama kina Riyad Mahrez, Pierre Emerick Aubamayeng au Achraf Hakimi, basi muda mrefu angechagua kucheza Ghana. Hata hivyo, alionekana sio bora kwa Wahispania ndio maana wakampanga mechi moja tu.
Vipi kwa Nico? Mzuri kama alivyo. Anateleza kule pembeni kama samaki katika mikono ya mwanadamu. Unamuona namna ambavyo anaisumbua michuano hii ya Euro? Wazungu walijua muda mrefu kwamba Nico ni mali. Wasingeruhusu acheze Afrika. Katika umri ambao alipaswa kuwa staa wa kikosi cha chini ya umri wa miaka 21 wao tayari walishampeleka timu ya wakubwa. Na hadi sasa katika umri huo anacheza kikosi cha wakubwa.
Wachezaji wengi wenye asili ya Afrika waliozaliwa Ulaya, huwa wanatudanganya kwamba wana mapenzi na bara hili pindi pale wanapokuwa wamekataliwa na timu za taifa za Ulaya. Wachache ndio wazalendo halisi. Nimewataja hapo juu.
Wengine wanakuja huku kwa sababu ni bidhaa ambazo zimekataliwa Ulaya. Mifano ya kina Inaki ipo mingi na hasa kwa hawa ndugu. Kumbuka rafiki zake Jerome Boateng na Kevin-Prince Boateng. Wote walizaliwa Ujerumani na baba Mghana.
Kuelekea Kombe la Dunia mwaka 2010 pale Afrika Kusini ghafla Wazungu wakaamua kutuachia Kevin-Prince halafu wakaondoka na Jerome. Kevin-Prince asingeweza kupasua katika kiungo cha Ujerumani cha kina Toni Kroos.
Mwenyewe alinyoosha mikono na kwenda kucheza kwao Ghana. Kama angekuwa na ubora kama wa mdogo wake ni wazi kwamba angecheza katika kikosi cha Ujerumani. Mara nyingi watoto wetu wanaozaliwa Ulaya chaguo lao la kwanza linakuwa kucheza timu za Ulaya.
Timu za Ulaya ndizo ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kushiriki Kombe la Dunia mara kwa mara. LakiniĀ zinawapa nafasi kubwa ya kushinda michuano ya Euro. Hapo hapo zinawapa nafasi kubwa ya kushinda Kombe la Dunia kuliko timu za Afrika. Hakuna timu ya Afrika iliyowahi kutwaa Kombe la Dunia achilia mbali kufika fainali.
Lakini watoto wengi wa Kiafrika waliozaliwa kule, hawa wale weusi, achana na hawa kina Hakimi wengi wanajiona wanatoka katika mataifa ya kule. Ni wazi kwamba Kevin-Prince Boateng anajiona ni Mjerumani zaidi kuliko Mghana.
Na kuna wengine ambao sio ndugu. Hawa ndio wengi zaidi. Hawa ndio kama rafiki yetu, Alex Tuanzebe. Majuzi tu ameamua kuichezea timu ya taifa ya DR Congo baada ya Waingereza kuona hawezi kuchezea taifa lao. Naamini hata yeye mwenyewe amejishtukia kuwa hawezi kuchezea England.
Rafiki yetu Yannick Bollasie naye ndio kama Tuanzebe. Aliamua kuichezea DR Congo baada ya kuona asingeweza kuichezea timu ya taifa ya England alikokulia au timu ya taifa ya Ufaransa ambako alizaliwa. Ni bahati kweli kuwapata wachezaji kama kina Kalidou Koulibaly ambao walizaliwa Ulaya, wakaonyesha uwezo wakiwa wadogo lakini bado wakachagua kuchezea timu za taifa za Afrika.
Ukitaka kulijua itazame timu ya taifa ya Ubelgiji. Imejaa wachezaji wengi wenye asili ya DR Congo ambao moja kwa moja kutokana na ubora wao waliamua kuichezea Ubelgiji. Tangu enzi za kina Mbo Mpenza na kaka yake, Emile Mpenza wote walianza kucheza Ubelgiji.
Baadaye zilipokuja zama za kina Vincent Kompany, Romelu Lukaku, Christian Benteke, Sambi Lokonga na wengineo wengi hawakujificha wakacheza zao kwa Wazungu. Ni kwa sababu ya ubora wao tu.
Wazungu wasingeweza kumruhusu Nico acheze katika asili ya kwao alikotokea. Wala wasingemruhusu Bukayo Saka akacheze Nigeria. Na hata wachezaji wenyewe wasingejiruhusu. Nadhani Waarabu ndio ambao wametunza mila za kucheza kwao kutokana na makuzi ya nyumbani kutojiona Wazungu sana. Ndio maana Wazungu hawakuwa na jinsi na badala yake hawakuweza kuwazuia kina Hakimi kucheza kwao.
Lakini kwa kiwango cha mchezaji kama Kobbie Mainoo, Wazungu wasingeweza kumruhusu akacheze Ghana. Wana watu wao ambao wanawajua mapema tu kwamba itakuwa mwiko kucheza nchi za asili zao.
Utaratibu wao ni uleule kama Wachina. Kuna bidhaa za kuleta Afrika na kuna bidhaa za kupeleka Ulaya. Ni kama walivyoamua kutuletea bidhaa yetu Inaki halafu wao wakaamua kubaki na Nico. Haishangazi kuona wakati mwingine ni ngumu kwetu pia kutoa mwanasoka mwingine bora wa dunia baada ya George Opong Weah. Kweli Wafaransa wangemruhusu Kylian Mbappe akacheze Cameroon?