Rombo. Wataalamu zaidi ya 25 kutoka Wizara ya Kilimo wanatarajiwa kupiga kambi katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, kutoa elimu ya namna bora ya kuzalisha zao la ndizi kwa kutumia umwagiliaji wa matone na kuachana na kilimo cha mazoea, ili kuzalisha kwa tija na kuuza bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.
Wilaya ya Rombo ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro ambazo zinazalisha zao la ndizi kwa wingi katika tarafa za Usseri, Tarakea, Mashati, Mkuu na Mengwe huku soko lake kubwa likiwa ni mikoa ya Dar es salaam, Dodoma pamoja na nchi za jirani.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Julai 6, 2024 katika kata ya Mengeni, mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kilimo hicho cha kisasa kitaleta tija kwa wakulima na kuwa na uhakika wa masoko.
Amesema mradi huo utatekelezwa katika kata za Mrao Keryo, Ushiri Ikwiini na kwamba watatumia Mto Ungwasi pamoja na maporomoko ya maji yaliyopo katika kata hizo ili wananchi walime kilimo hicho cha kisasa na chenye tija na wakulima wataweza kuuza ndizi mbivu na mbichi nchi jirani.
“Kupitia kilimo hiki cha matone, tutaruhusu wakulima kuwa na migomba ya kisasa kwa ushirikishwaji kwa watu wote, zikiwemo taasisi za dini, watu wanaweza wasing’oe migomba wakatenga robo shamba au nusu shamba kwa ajili ya kilimo hiki cha matone,” amesema Profesa Mkenda.
“Watakuja wataalamu 25 kutoka Wizara ya Kilimo kupiga kambi hapa, kuja kufanya umwagiliaji wa matone ili kuongeza kipato cha wakulima katika kata za Ushiri Ikwiini na Mrao Keryo, tutatumia Mto Ungwasi na maporomoko ya maji yaliyopo,” amesema Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda ameishukuru Wizara ya Kilimo kupitia waziri wake, Hussein Bashe kwa kutoa wataalamu hao kwenda kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kutumia kilimo hicho cha matone.
Agripina Oisso, mmoja wananchi wa wilaya hiyo, amesema kilimo hicho kitakuwa ni mkombozi kwa wakulima na kwamba wataweza kuzalisha kwa tija kwa kuwa na bidhaa bora ambazo zitauzika kimataifa.
“Huu utaratibu umekuja kwa wakati mwafaka sana, mpango huu tunaamini utaenda kumkomboa mkulima kwa kuwa tutazalisha bidhaa zenye ubora, hivyo tunaamini tutapata masoko ya uhakika kuuza bidhaa zetu,” amesema Agripina.