Dar es Salaam. Ni jambo la kawaida kwa mwanamume kuota ndevu na ni ishara ya hatua ya ukuaji. Hii ni tofauti na mwanamke kuwa na ndevu ambapo tafsiri huwa tofauti.
Mwanamke mwenye ndevu huibua maswali kwa jamii kuhusu sababu ya muonekano wake, jambo ambalo humfanya mhusika kutojiamini.
Kutojiamini huku, huwafanya wanawake wenye hali hiyo kutafuta njia mbalimbali kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kunyoa, kutumia dawa na vipodozi vya kuondoa ndevu.
Wanapoota ndevu nyingi hukabiliwa na changamoto za kisaikolojia kutokana na kuwa na mwonekano kama wa wanaume.
Mitazamo na mila nyingi za kijamii katika Bara la Afrika, bado zinakumbatia unyanyapaa wa wazi au wa kificho kwa wasichana wanaoota ndevu nyingi.
“Zilianza miaka mitano iliyopita, siku moja nikiwa darasani nilianza kuchezea shingo yangu wakati namsikiliza mwalimu. Ghafla nikahisi kushika kitu kama nywele ndefu na niliposhika vizuri nikashangaa kuhisi ni nywele.
“Nilitoka haraka kwenda bafuni kuangalia kwenye kioo, nikabaini ndevu. Niliendelea kuichezea siku moja nikaing’oa, baadaye zikaanza kuota nyingine na mpaka sasa ninazo nyingi,” anasimulia Rehema Juma (26).
Lightness Richard (45) anasema baada ya kuona viashiria vya kuotwa na ndevu alianza kwa kuzing’oa na baada ya muda zikaongezeka.
“Sasa ndevu zilianza kuota chache, kadiri nilivyong’oa ndivyo zilivyoongezeka, sasa hivi nanyoa maana ni nyingi, wakati zinaanza niliambiwa nitakuwa na fedha nyingi, mara nina shida ya homoni, ili kuondoa hayo maneno nimekuwa nikinyoa mara kwa mara zisionekane,” anasema.
Lightness anasema kwa sasa anatafuta matibabu kwa sababu kadiri muda unavyokwenda ndivyo zinavyoongezeka.
Miaka ya nyuma anasema aliwahi kupata tatizo la uvimbe kwenye kizazi, ambalo wataalamu wanaeleza ni sababu mojawapo ya mwanamke kuwa na ndevu.
Daktari na Mratibu wa idara ya utafiti na mafunzo, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Ernest Winchislaus anasema kunyoa ndevu kwa mwanamke kunazifanya ziongezeke.
“Unaponyoa unachochea ukuaji wa haraka wa ndevu, kuna namna wataalamu tunashauri kukabiliana na tatizo, ikiwemo kutumia dawa au kubadili mfumo wa maisha,” anasema.
Dk Winchislaus anasema mara nyingi wanawake wanaokuwa na ndevu hukumbwa na changamoto ya kutojiamini, hali ambayo huibua msongo wa mawazo.
Moja ya sababu za wanawake kuota ndevu ni dosari za ulinganifu katika mfumo wa vichocheo vya mwili, hasa vile vinavyoamua kutokea kwa mabadiliko ya ukuzi wa kijinsia.
Dosari za ulinganifu wa vichocheo vya kijinsia kwa wasichana zinaweza kusababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuzalishwa kwa wingi kwa vichocheo vya ujinsia, kutoka katika mifuko ya mayai na uvimbe katika mifuko ya mayai.
Sababu ya kwanza anayoielezea Dk Winchislaus juu ya kuota kwa ndevu kwa mwanamke, mosi ni ongezekezo la homoni ya kiume katika mwili ambayo huchagizwa na sababu nyingi.
Anasema homoni ya kiume inapokuwa nyingi kwenye mwili wa mwanamke, mtu husika huanza kupata tabia za kiume, ikiwemo kuwa na sauti nzito pamoja na kuota ndevu.
Pia Dk Winchislaus anasema mwanamke kuwa na vivimbe vidogo kwenye ovari huchangia hali hiyo.
“Hali hii hutokea pale ovari za mwanamke zinapokuwa na vivimbe vidogovidogo ambavyo huongeza uzalishaji wa homoni ya kiume, asilimia mpaka 75 ya wanawake wenye tatizo la ukuaji wa ndevu huwa na ugonjwa huu,” anaeleza.
Kundi linaloathiriwa zaidi, Dk Winchislaus anasema ni mabinti walio katika umri wa kuvunja ungo.
Chanzo kingine ni kijenetiki, anasema sababu hizi kwa baadhi ya watu kwenye familia hurithi hali hiyo kutoka kwa ndugu.
“Hii inamaanisha kama mama au dada wa mwanamke ana ndevu, anaweza pia kuwa na uwezekano wa kuwa na hali hiyo,” anasema.
Daktari huyo pia anataja matumizi ya dawa kusababisha ukuaji wa nywele usoni. Mfano dawa za kuongeza misuli huchangia tatizo hilo pamoja na dawa nyingine zinazohusiana na homoni.
Matumizi ya dawa za kupanga uzazi, Dk Rajeshwari anasema zinachochea pia ukuaji wa kasi wa nywele, hii hutokana na athari zake kwenye homoni za kike mwilini.
Mtaalamu wa fiziolojia ya homoni, Dk Chour de Garang anasema muhimu ni mwanamke kujua sababu au chanzo cha ndevu kuota ni nini.
“Matibabu yataendana na chanzo, mfano kwa wale wenye uzito mkubwa, kupunguza uzito kwa njia ya aina ya chakula, mazoezi, lakini muhimu zaidi kwenda kwa wataalamu wajue aina ya mazoezi na kiasi kinachohitajika kwa siku au wiki,” anasema Garang.
Katika utafiti uliowahusisha wanawake 102 wanaokabiliwa na tatizo la kushindwa kutunga mimba waliohudhuria katika kliniki ya magonjwa ya wanawake, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kati ya Septemba 2006 na Februari 2007, ilibainika miongoni mwao asilimia 32 walikuwa na uvimbe katika mifuko ya mayai.
Asilimia 56.3 ya wanawake wote wenye uvimbe huo, walikuwa na tatizo la kuwa na nywele nyingi mwilini, ikiwa ni pamoja na kuota ndevu.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Dk Pembe AB na Abeid MS wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili (Muhas), uliochapishwa katika Jarida la Kisayansi la Tanzania, Journal of Health Research la Oktoba 2009.
Utafiti ulibaini kuwa mambo mengine yanayochangia kutokea kwa tatizo hili ni matumizi ya dawa za hospitalini na vipodozi vyenye viambata vya dawa kama testosterone na steroid.
Kuwa na ndevu kupitia utafiti huo ilionekana ni matokeo ya matumizi ya muda mrefu ya kutumia vipodozi hivyo, bila kupata ushauri wa afya.