Sabasaba yamkumbusha Kikwete enzi za utawala wake

Dar es Salaam. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) yamekuwa ya kipekee kwa kuboreshwa miundombinu, hususani ya barabara tofauti na miaka ya nyuma.

Kikwete ameeleza hayo leo Julai 6, 2024 alipotembelea maonyesho hayo maarufu Sabasaba.

Katika mazungumzo yake alikuwa akilinganisha hali anayoiona na miaka ya nyuma, hususani wakati wa utawala wake.

“Kipindi changu wakati nakuja barabara zilikuwa za vumbi na maombi yangu yalikuwa ni kuhakikisha barabara zinawekwa lami maana ilikuwa unakuja huna mafua lakini unaondoka na mafua,” amesema.

Pia amesema alikuwa anaangalia uboreshaji wa mabanda na bidhaa zinazoonyeshwa kuanzia kwa wageni hadi wazawa na hata waelekezaji wamekuwa wakieleza kitu kwa ufasaha tofauti na miaka ya nyuma.

Akizungumzia nishati safi, Kikwete amesema wakati anapokea uongozi matumizi ya umeme yalikuwa asilimia 10 na matumizi makubwa yalikuwa mjini na siyo kijiji.

Amesema waliamua kuanzisha mradi wa umeme vijijini ambao ulianzia kwa hayati Rais Benjamin Mkapa na yeye alilikamilisha na alipokwenda kwenye ziara mkoani Mara alizindua umeme vijijini na wakati huo ukiwa kwenye vijiji 206.

Wakati huo watu walikuwa wanahitaji umeme vijijini na wangeachiwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao wanafanya biashara wao wanaangalia sehemu ambayo walikuwa na uhakika wa biashara.

Kikwete ametoa wito kwa watoa huduma wa umeme na gesi kuangalia bei wanazotoza zisiwaumize watumiaji kwani inaweza kuwa sababu ya kurudi kwenye matumizi ya mkaa na kuni.

“Sijui kama takwimu zimebadilika Dar es Salaam walikuwa wanatumia magunia ya mkaa 40,000 kwa siku ni kwa kiasi gani miti imepotea hapo,” amehoji.

Kikwete ametumia zaidi ya saa tano kuzunguka viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa.

Aliingia uwanjani saa 5.30 asubuhi na hadi saa 11.00 jioni alikuwa bado akizunguka kwenye mabanda kuangalia bidhaa, kununua na kuacha maoni katika baadhi ya sehemu alizotembelea.

Related Posts