Dar es Salaam. Edger Mwakabela aliyetekwa na watu wasiojulikana na kutupwa kwenye pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwilini, ameruhusiwa kutoka hospitali.
Ruhusa hiyo ni baada ya kufanyiwa upasuaji wa taya la kushoto Julai 3,2024, lililosagika kwa kudaiwa kupigwa risasi na watekaji ambao walilenga kumpiga risasi ya kichwa.
Mwakabela maarufu Sativa kupitia mtandao wa X alipatikana Juni 27, akivuja damu baada ya kuteswa na watu wanaodaiwa kumteka.
Baada ya kupatikana Sativa alilalamika maumivu ya kichwa, miguu na mikono iliyokuwa na michubuko ya panga.
Kijana huyo mkazi wa Mbezi anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha, alifanyiwa upasuaji hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kupata mpasuko wa taya la kushoto.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 6, 2024 mratibu wa matibabu ya Sativa, Martin Masese maarufu ‘MMM’, amesema sativa ameruhusiwa kurudi nyumbani na atatakiwa kurejea kliniki baada ya siku saba.
“Atarudi kliniki baada ya siku saba, baada ya siku 14 pia atarudi akaondolewe nyaya kwenye taya lake,” amesema Martin.
Kwa upande wake, Wakili wa Sativa Paul Kisabo kupitia mtandao wake wa X alikoweka picha akiwa na Sativa ameandika: “Tunawashukuru madaktari waliomtibu,@Sativa25, tuendelee kumuombea.
Kwa sasa ataendelea na kliniki Aga Khan Hospital. Tunahitaji tume huru iundwe ili kuchunguza na kuhakikisha wahusika wote waliomteka, kumtesa na kumpiga risasi wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” ameandika Wakili Kisabo kupitia mtandao wake wa X.
Sativa aliyetoweka Juni 23, alipatikana baada ya marafiki na wanaharakati kupitia mitandao ya kijamii kupaza sauti ya kutekwa kwake na watu wasiojulikana.
Julai 27 kijana huyo alipatikana mkoani Katavi ndani ya pori la hifadhi.
Sativa alieleza kuwa, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana walimpeleka mkoani Arusha na baadaye kusafirishwa hadi mkoani Katavi.
Kupitia video ilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Sativa alionekana mkoani Katavi akiwa ameokotwa na wasamaria wema na kutapakaa damu usoni, akiomba msaada kupelekwa hospitali.