TANZANIA imepangwa katika kundi H la mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco. Mechi hizo za makundi zitaanza kupigwa kati ya Septemba 2 hadi Novemba 19, 2024 kabla ya fainali kupigwa mapema mwakani.
Katika kundi hilo ililopangwa Taifa Stars sambamba na timu za taifa za DR Congo, Guinea na Ethiopia na ili ifuzu Afcon inapaswa kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo vinginevyo Watanzania watalazimika kutazama mechi za fainali hizo kupitia runinga.
Ni kundi ambalo limeshikilia ndoto ya Tanzania kushiriki Afcon kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushiriki zilizopita lakini pia kufuzu mashindano hayo yenye thamani kubwa zaidi barani Afrika kwa mara ya nne baada ya kushiriki fainali za 1980, 2019 na 2023.
Haionekani kama itakuwa kazi rahisi kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kufuzu fainali hizo za mwakani kutokana na ubora na aina ya timu ambazo imepangwa nazo pamoja katika kundi hilo.
Ubora wa kitimu na mchezaji mmojammoja pamoja na uwepo wa makocha wa daraja la juu ni silaha kubwa ambayo Taifa Stars inapaswa kuwa makini nayo dhidi ya DR Congo na Guinea katika harakati hizo za kuisaka safari ya Morocco mwakani. Ethiopia haipaswi kuonekana kama mpinzani rahisi kwa vile inatoka katika kanda moja ya soka na Tanzania ambayo ni ile iliyo chini ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), hivyo ina uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania na wachezaji wake kwa muda mrefu pamoja na mazingira.
Na ikumbukwe pia timu ya DR Congo ina wachezaji ambao wanafahamiana vyema na wale wa Kitanzania kwa vile wamewahi kucheza hapa nchini.
Tathmini ya dondoo za timu hizo tatu ambazo zimepangwa katika kundi moja na Taifa Stars inaweza kutoa picha ya uzito wa mzigo ambao timu hiyo inao dhidi ya Guinea, DR Congo na Ethiopia katika vita ya kuwania kufuzu Afcon awamu ijayo.
Katika hafla ya upangaji makundi ya kuwania kufuzu Afcon 2025 iliyofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, juzi Alhamisi, DR Congo ilikuwa katika chungu cha kwanza ambacho kilijumuisha timu 12 bora zaidi barani Afrika kwa mujibu wa viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) vya mwezi Juni.
Maana yake ni timu ambayo kwenye makaratasi inapewa nafasi kubwa ya kufuzu kupitia kundi H mbele ya Guinea, Tanzania na Ethiopia.
Katika kundi H, DR Congo ndio timu ambayo imeshiriki mara nyingi zaidi katika fainali za Afcon ambapo imefanya hivyo mara 20 na ikiwa itafanya hivyo safari hii itashiriki kwa mara ya 21. Lakini ndio timu yenye mafanikio zaidi kwenye Afcon mbele ya Guinea, Ethiopia na Tanzania kwa vile imetwaa ubingwa mara mbili, imeshika nafasi ya tatu mara mbili na ilimaliza katika nafasi ya nne mara mbili.
Taifa Stars imekuwa haina historia nzuri dhidi ya DR Congo katika mechi za mashindano ambapo katika mara saba ambazo zimewahi kukutana kwenye mashindano tofauti imepata ushindi mara moja, imetoka sare mara tatu na kupoteza michezo mitatu.
Timu hiyo inayonolewa na kocha Mfaransa Sebastien Desabre kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com ina kikosi chenye thamani ya Euro 115.60 milioni (takriban Sh331.7 bilioni) na mchezaji ghali zaidi ni winga Yoane Wissa anayechezea Brentford inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL) akiwa na thamani ya Euro 28 milioni (takriban Sh80 bilioni).
Kwa mujibu wa viwango vya ubora wa Fifa kwa mwezi Juni, Guinea ambayo inatoka katika kanda ya soka ya Afrika Magharibi (Wafu) ipo nafasi ya 77 na katika uchezeshaji wa droo ya kuwania kufuzu Afcon ilikuwa katika chungu cha pili.
Imekuwa na uzoefu wa kutosha katika ushiriki wa fainali za Afcon na katika kundi H ipo nafasi ya pili kwa kushiriki mara nyingi nyuma ya DR Congo ikiwa imefanya hivyo mara 11.
Mafanikio makubwa ambayo Guinea imeyapata katika fainali za Afcon ni kumaliza katika nafasi ya pili ikifanya hivyo mwaka 1976 huku bingwa ikiwa ni timu ya taifa ya Morocco.
Timu hiyo kwa sasa inanolewa na nyota wake wa zamani, Kaba Diawara na kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com, kikosi chake kina thamani ya Euro 69.53 milioni (Sh199.5 bilioni). Katika mechi za mashindano Guinea na Tanzania zimekutana mara moja katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2 lakini kiujumla zimekutana mara tatu, mbili zikiwa za kirafiki na zote Guinea ilipata ushindi.
Serhou Guirassy anayeichezea VfB Stuttgart inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ndiye mchezaji ghali zaidi katika kikosi cha Guinea akiwa na thamani ya Euro 40milioni (Sh115 bilioni).
Ethiopia ni miongoni mwa timu zenye historia ya kuwahi kutwaa ubingwa wa fainali za Afcon ikifanya hivyo mara moja katika fainali za mwaka 1962 ilipoichapa Misri kwa mabao 4-2 katika mechi ya fainali.
Imewahi kumaliza katika nafasi ya pili mara moja ambayo ilikuwa ni mwaka 1957, mwaka 1959 ikishika nafasi ya tatu na katika fainali za 1963 na 1968 ilimaliza katika nafasi ya nne.
Timu hiyo inanolewa na kocha mzawa, Gebremedhin Haile mwenye umri wa miaka 57 ambaye alianza kuitumikia nafasi yake mwaka jana akirithi mikoba ya Daniel Gebremariam aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu Afcon.
Kikosi cha Ethiopia kinaundwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka nchini mwao na nahodha wake ni kiungo mkabaji, Gatoch Panom ambaye anaitumikia Fasil Kenema.
Kihistoria timu hizo zimekutana mara 18 katika mechi za mashindano tofauti ambapo Tanzania imeibuka na ushindi mara nne, zimetoka sare saba na Ethiopia imepata ushindi katika mechi saba.