Tabora. Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu wasiofahamika wameyavamia na kuyavunja makaburi 19 yaliyopo Mtaa wa Magubiko kata ya Kiloleni Manispaa ya Tabora, huku tabia hiyo ikitajwa kuwa imekuwa ya ikijirudia kwa matukio tofauti yanayofanana na hilo.
Alexander Ntonge aliyezika ndugu yake hivi karibuni, amesema yeye alipigiwa simu kuwa umetokea uharibifu wa kuvunjwa makaburi na kwamba kaburi la babu yake limebomolewa.
“Nilipigiwa simu kwamba kuna uharibifu wa makaburi kwa kuwa nipo hapa Tabora haraka nikafika na kushuhudia makaburi yote yaliyokuwa na vigae yamebomolewa bila sababu na hawajabomoa kaburi moja wamebomoa mengi. Hali hii imenishangaza sana kwa kuwa imetokea makaburi mengi kuvunjwa jambo ambalo linaleta hasara kwa ndugu kuanza kujenga upya makaburi”
Naye Revocatus Sunga, mkazi wa Kiloleni ambaye kaburi la baba yake limeharibiwa na wahalifu hao, amesema ameumizwa na uharibifu huo kwa kuwa kaburi ni la baba yake mzazi na maziko yamefanyika miezi michache iliyopita.
“Tumepoteza mtu na sasa tuanze tena gharama upya za kulijengea, hii inatia simanzi sana maana vitu walivyochukua hapa wanavipeleka kwenye vyuma chakavu hata ukiviangalia havina thamani hata kidogo. Naziomba mamlaka kuhakikisha waliofanya haya wanakamatwa maana hii ikiachwa itaendelea na italeta madhara zaidi,”amesema.
Mwananchi mmoja anayeishi jirani na makaburi hayo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, amesema wakati tukio hilo linafanyika alisikia lakini aliogopa kutoka nje kutokana na hofu.
“Ilikuwa kama kuna nyumba inabomolewa hivi, kwa kuwa nyundo zilikuwa kubwa na kishindo kilikuwa kikubwa, lakini nilihofia na hata walinzi ambao walikua jirani nao walihofia, hatukujua walikuwa wangapi,” amesema.
Diwani wa kata hiyo, Mapambano Shaban amesema tukio hilo linadaiwa kufanyika usiku wa kuamkia Julai 5 mwaka huu.
“Baada ya kupata taarifa hizo nikatoka na mtendaji wangu wa kata kwenda kujionea, baada ya kufika tukakuta zaidi ya makaburi 19 yamebomolewa na kikubwa walikuwa wanachukua vyuma vya aluminiamu.
“Tukio hili sio mara ya kwanza kutokea, nakumbuka miezi mitatu iliyopita kuna kundi lilitokea na kuanza kuchukua misalaba ya chuma kwenye makaburi na kwenda kuiuza kwenye vyuma chakavu, wale walikamatwa na wengi wao walifungwa na hali ikatulia, sasa wameanza tena hivyo tunaanza msako wa kuhakikisha wanakamatwa,”amesema.
Peter Kubingwa ni mwenyekiti wa mtaa wa Magubiko kata ya Kiloleni amesema vitendo hivyo ni vya kusikitisha.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema: “Nimepata taarifa za makaburi kuvunjwa na watu ambao hawajafahamika, tayari uchunguzi unaendelea ili tuwabaini waliofanya uhalifu huo na kisha hatua kali dhidi yao zichukuliwe.”