TAWA yakaribisha Watanzania, wageni kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iimetoa wito kwa Watanzania na wageni kuwekeza kwenye sekta ya utalii ili kujiongezea kipato na kuchangia pato la Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Afisa utalii, Daud Tesha kutoka TAWA wakati akizungumza na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili leo tarehe 6 Juni 2024 katika viwanja vya maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara ‘Sabasaba’ yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Amesema ndani ya TAWA zipo fursa zinalenga kuhamasisha umma wa watanzania, wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza kwenye sekta ya utalii.

Amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika taasisi hiyo

Akizitaja fursa hizo Tesha maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), uwindaji wa kitalii na ufugaji wa wanyamapori.

“TAWA imetenga maeneo kadhaa kwa ajili ya kufanya shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere. Eneo hilo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10, hutoa burudani safi kwa watalii” amesema Tesha.

“Maeneo mengine ni Pori  la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO, Ruhila ZOO, Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo kujenga kambi za kulala wageni (Campsites), hosteli, lodge na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (Picnic Sites),” ameongeza.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ametumia  fursa hiyo kuwakaribisha wananchi Wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

Kama kauli mbiu ya maonesho hayo inavyosema kuwa ‘Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji,’, Tesha ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizo zilizopo TAWA kwa sababu ni taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji.

“Pia wanaweza katika mashamba ya wanyamapori, bustani za wanyamapori nk.” amesema Maganja

“Hii ni fursa adhimu kwa wawekezaji wote kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu,” ameongeza.

Maonesho hayo yanayoendelea jijini Dar es Salaam, yameanza tarehe 28 Juni 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 14 Julai 2024.

Related Posts