Tawa yanadi fursa za uwekezaji maonesho ya Sabasaba

Na Beatus Maganja, Dar es Salaam.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatumia maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam kuhamasisha Watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia.

Akizungumza na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Afisa Utalii, Daud Tesha, amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji kuwekeza katika taasisi hiyo.

Tesha amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika taasisi hiyo kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), uwindaji wa kitalii na ufugaji wa wanyamapori.

“TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi kwa watalii,” amesema Tesha.

“Maeneo mengine ni Pori la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO, Ruhila ZOO, Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni (Campsites), Hosteli, Loji na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (Picnic Sites),” amesema.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

“Kama kaulimbiu ya maonesho haya inavyosema kuwa Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji, nitumie fursa hii kuwaambia Watanzania wote kuwa TAWA ni Taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji kwani inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali kama vile ujenzi wa nyumba za wageni, kumbi za mikutano katika maeneo yetu, kambi za watalii, michezo ya watoto. Mwekezaji anaweza akatumia fursa ya kuwekeza katika mashamba ya wanyamapori, bustani za wanyamapori na mengine.

“Kwahiyo hii ni fursa adhimu kwa wawekezaji wote kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu,” amesema Maganja.

Maonesho hayo yenye Kaulimbiu “Tanzania ni Mahali Salama Pa Biashara na Uwekezaji” yameanza 28 Juni, 2024 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2024.

Related Posts