KIUNGO aliyekuwa akikipiga Ihefu (sasa Singida Black Stars), Duke Abuya inaelezwa yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Coastal Union itakayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Inadaiwa Abuya aliyemaliza mkataba na Singida ni pendekezo la kocha David Ouma akitaka kuibeba timu katika michuno ya CAF kwa uzoefu alionao.
SINGIDA Black Stars, unadaiwa kuridhia kutomuongezea mkataba mpya aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Ezekiel Mwashilindi msimu ujao.
Nyota huyo inaelezwa siyo chaguo la Kocha Patrick Aussems aliyependekeza asiongezewe mkataba mpya, huku ikielezwa huenda akaibukia chama lake la zamani la Tanzania Prisons.
KLABU ya Tanzania Prisons, imeanza mazungumzo ya kupata uhamisho wa kiungo mshambuliaji wa Pamba Jiji, Ismail Ally msimu ujao.
Kiungo huyo aliyefunga mabao sita na kuasisti manane msimu uliopita wa Ligi ya Championship akiwa na Pamba, ni kati ya wachezaji waliomvutia Kocha Mbwana Makata anayemhitaji akafanye naye tena kazi.
WINGA wa kimataifa wa Madagascar, Tendry Mataniah anahusishwa kujiunga na mojawapo wa vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga.
Nje na watani hao wa jadi, klabu ya AS Vita ni miongoni mwa timu zinazowania saini ya winga huyo mwenye umri wa miaka 26 aliyekuwa akikipiga CNaPS Sport.
DODOMA Jiji ipo katika hatua za mwisho kumalizana na beki Mkongomani, Pascal Kitenge ambaye amewahi kuzichezea timu mbalimbali hapa nchini.
Beki huyo aliwahi kuzichezea klabu kadhaa nchini ikiwemo Stand United, Coastal Union na Mtibwa Sugar, lakini sasa ametua katika rada za wenyeji hao wa Jiji la Dodoma.
KATIKA kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Mashujaa Queens imeanza mazungumzo na kipa wa Yanga Princess, Husna Mtunda ili kumnyakua akakipigie kwa maafande hao.
Mtunda amesalia na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Yanga na Mashujaa imeweka nia ya kuuvunja ili kuinasa saini yake.
KLABU ya She Cooperate ya Uganda imevutiwa na kiwango cha beki wa kati wa Yanga Princess, Masika Mwakisua.
Timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Uganda inaelezwa kuwa kama kila kitu kitakwenda sawa Masika atakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao.