TETESI ZA USAJILI BONGO: Moloko, Namungo kuna jambo linakuja

UNAMKUMBUKA yule winga teleza wa zamani wa Yanga, Jesus Moloko? Unaambiwa jamaa baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao na klabu ya Al Sadaqa SC ya Libya, kwa sasa anajiandaa kurudi tena Bongo.

Inadaiwa kuwa winga huyo aliyeachwa msimu uliopita na Yanga anajiandaa kutua Namungo ambayo imekuwa ikiwasiliana na kufanya naye mazungumzo na Moloko.

Mchezaji huyo alitimkia Libya baada ya kumalizana na Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili akitwaa nayo mataji saba ikiwamo Kombe la Mapinduzi, mawili ya Ligi Kuu Bara na mengine kama hayo ya Kombe la Shirikisho pamoja na Ngao ya Jamii. Moloko alikuwa kikosi cha moto kilichoirejeshea Yanga furaha.

COASTAL Union imeanza mazungumzo na Kariobangi Sharks ya Kenya ili kupata saini ya nyota mshambuliaji, John Mark Makwata. Coastal itakayoshiriki michuano ya CAF, inataka kukamilisha dili hilo baada ya kuvutiwa na Makwata ambaye msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Kenya, alifunga mabao 16 katika michezo 13 aliyocheza.

KIPA namba moja wa Tanzania Prisons aliyekuwa akiwindwa na Yanga, Yona Amos inaelezwa amenaswa na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Pamba Jiji.

Amos aliyekuwa akitajwa kwenda kuziba nafasi ya Metacha Mnata wa Yanga, anadaiwa kutua Pamba ili kutumia uzoefu wake kuibeba timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu.

Related Posts