NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
CHUO Kikuu Cha Dar Es Salaam, Ndaki ya TEHAMA wamebuni mfumo joto unaojiendesha kwa kujiongeza na kujipunguza joto kulingana na uhitaji wa wakati husika kwenye uhifadhi vyakula pamoja na kufuga kuku wa kisasa (broila).
Akizungumza leo Julai 5,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa Sabasaba Jijini Dar es salaam Mhandisi wa Maabara, Ndaki ya Tehama Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Adriano Kamoye amesema kuku wa kisasa (broila) katika ukuaji wake wanahitaji joto kulingana na ukuaji wake.
“Katika ukuaji wa kuku wa kisasa, joto ni kitu cha muhimu sana, wafugaji wengi hutumia taa pamoja na mkaa, njia ambayo si salama katka ukuaji wa kuku hao, ndo maana tukaamua kuja na mfumo huu wa kisasa ambao ni bora na ni salama kwenye ufugaji” amesema
Aidha amesema kuwa Mfumo huo pia unaweza kutumika katika kuhifadhi mazao wakati wa usafirishaji na utunzaji kwa lengo la kuhifadhi ubora wa matunda au mbogamboga.
“Mbogamboga zinahitaji unyevunyevu wa kiasi fulani ili kuhifadhi ubora wake kwa muda mrefu, kwahiyo unyevunyevu ukiwa mkubwa au mdogo unaweza poteza ubora wake, kwahiyo mfumo huu unaweza kutuma katika mazingira hayo kutunza ubora wa matunda au mbogamboga”amesema.