Veta yatengeneza mtaala kufundisha wafanyakazi wa ndani

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema imetengeneza mtaala kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kuhudumia wazee na kazi za nyumbani kutokana na kuwapo kwa hitaji katika soko la ajira.

Akizungumza leo Julai 6,2024 Julai 6,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore, amesema mitaala hiyo imetengenezwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kazi hizo zitambulike rasmi.

“Kuna maeneo mawili watu walikuwa wanahitaji tuyatolee ujuzi; kutoa ujuzi kwa wenzetu wanaofanya kazi za ndani na wanaohudumia wazee. Tumeshirikiana na wadau tumetengeneza mtaala utakaowasaidia Watanzania kupata ujuzi wa kwenda kuwahudumia wazee, watoto na kufanya shughuli za nyumbani…hadi kupika mtu anafundishwa.

“Tumefanya hivi kwa sababu tunaona kuna Watanzania ambao wanahitaji kwenda nje ya nchi kufanya kazi, kutambulika na ujuzi unaohitajika ndiyo maana tuliamua kutoa mafunzo haya,” amesema Kasore.

Amesema mtaala mwingine unahusu utengenezaji wa vifaa tiba mbalimbali ambapo kozi hiyo imeanza kutolewa katika vyuo vya Veta Geita na Musoma.

“Tumeona kuna wawekezaji wanakuja nchini, tumekuja na mtaala na kozi ambayo inawalenga wale wanaokwenda kufanya kazi kwenye maeneo ya viwanda ambayo imeanza tangu Desemba mwaka 2023. Viwanda vinatumia mitambo, kompyuta hivyo, kozi hii itawasaidia,” amesema.

Amesema mbali ya kuwapatia watu ujuzi pia wanawahamasisha wanafunzi kuja na mawazo ya kibunifu yatakayotoa suluhisho kwa jamii.

Aidha amesema wanatumia maonesho hayo kuonyesha huduma wanazozitoa katika vyuo mbalimbali vya Veta zikiwemo kozi zinazotolewa kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu.

“Tunaonyesha aina ya mafunzo tunayoyatoa na Watanzania wengi wanajua wakija Veta watapata ujuzi, watafundishwa na kwa sasa tunatoa ujuzi zaidi katika maeneo mbalimbali. Tunafundisha watu wenye mahitaji maalumu…unayemuona hawezekani tunakwenda kumtengeneza na atakwenda kufanya shughuli mbalimbali,” amesema Kasore.

Kwa mujibu wa Kasore, vyuo vya Veta vimeongezeka kutoka 22 na kwa sasa vimefikia 80 katika mikoa na wilaya na kwamba ujenzi wa vyuo 65 unaendelea kikiwemo cha Mkoa wa Songwe.

Related Posts