Vyama vya ushirika vyatakiwa kuboresha huduma kwa wanaushirika

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amevitaka vyama vya ushirika kubuni mbinu mpya zitakazowezesha wakulima kupata huduma, pembejeo na bei bora za mazao yao ili kuchochea maendeleo.

Dkt. Biteko amesema hayo leo tarehe 6 Julai, 2024 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani – SUD yaliyofanyika katika Viwanja vya Ipuli mkoani Tabora.

Amesema umefika wakati wa kufanya mabadiliko ya dhati katika sekta ya Kilimo na kuondokana na michakato na maoni yasiyo na tija ambayo huchelewesha maendeleo.

Amevitaka vyama vya ushirika na wanunuzi wa mazao kuhakikisha wanarejesha rasrilimali kwa wananchi kupitia CSR ili maendeleo katika maeneo husika yaendane na rasiriamali zinazopatikana katika maeneo hayo.

Aidha, ameagiza viongozi ngazi ya mikoa, Halmashauri na Serikali za mitaa kuwatumia maafisa ushirika kikamilifu ili mchango wao uwe na tija kwa maendeleo ya Nchi.

“Watanzania zaidi ya milioni nane wanaotegemea sekta ya ushirika wanahitaji huduma. Hivyo watumie maafisa Ushirika kubuni na kushauri kitaalam namna bora ya kuwafikia walengwa” amesema Dkt. Biteko.

Amesema katika kufanikisha azma hiyo, yapo mazingira wezeshi kwa vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa vinapanga kuanzisha Benki ya Taifa yenye lengo kuwezesha upatikanaji wa mitaji yenye masharti nafuu kwa wanaushirika.

Dkt. Biteko amewapongeza kwa jinsi wanavyosimamia na kuwezesha wakulima kupata pembejeo, mikopo, kuzalisha na kupata masoko yenye bei nzuri kwa wakulima nchini.

“Hivi karibuni tumeona masoko ya mazao ya wakulima hususan mazao ya Kahawa, Pamba, Ufuta, Mbaazi, Korosho na Kokoa yakiimarika na kuwavutia wakulima wengi kuzalisha,” ameongeza Dkt. Biteko.

Vilevile, Dkt. Biteko ameelezea kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa pembejeo zinawafikia wakulima kwa bei ya kuridhisha, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwa wawekezaji wa pembejeo hapanchini.

Naye, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa msaada wa kifedha kwa ajili ya pembejeo za kilimo, ikiwemo tumbaku, pamba na korosho, ili kuwawezesha wakulima kufanya shughuli zao kwa urahisi na ustawi.

Amesema jitihada za Serikali kufuatilia na kuweka ukomo wa bei kwa mazao mbalimbali zitaendelea kutiliwa mkazo.
“Kumekuwa na ongezeko la bei ya mazao na tutahakikisha bei ya mazao haishuki” amesema Waziri Bashe.

Amesema Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 13 kwa wakulima wa Tumbaku na zaidi ya shilingi bilioni 13.3 ikiwa ni gharama ya pembejeo kwa wakulima wa tumbaku.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Abdulmajid Nsekela amesema tume inaendelea kuwasimamia washirika kuleta tija kwa wananchi.

Akizungumzia ujenzi na uendeshaji wa Benki ya Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege amesema Makao Makuu ya Benki hiyo yatakuwa Dodoma ili kurahisisha wananchi wote na washirikia kufika kwa urahisi na itakuwa na matawi katika mikoa minne kwa kuanzia.

Ameongeza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuhamasisha wanachama kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi na kuhusisha wadau wengine wanaofanya kazi na vyama vya ushirika.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini Charles Jishuli, amesema Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yamefanyika kwa miaka 23 hadi sasa.

Ameiomba Serikali kushirikiana na ushirika katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ili iwe na manufaa.

.

.
.
.
.
.

Related Posts