Dar es Salaam. Baadhi ya wataalam wa masuala ya biashara wameelezea wasiwasi wao kuhusu kukosekana kwa tafiti zinaoshughulikia changamoto nyingi zinazowakabili wafanyabiashara ikiwemo jinsi ya kujiendesha katika teknolojia.
“Tuna vyuo vikuu vingi, lakini matokeo mengi ya tafiti zao hayapatikani kwa urahisi kwa wale wanaohitaji ufumbuzi wa changamoto zao za biashara,’’ amesema mtaalamu wa uchumi Dk Tumaini Msolwa.
Msolwa ameyasema hayo Julai 5, 2024 jijini hapa katika maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Amebainisha kuwa wafanyabiashara wengi wanashindwa kufanya vizuri sokoni, kwa sababu walitegemea maarifa yao wenyewe au ushauri usio wa kitaalamu kuingia kwenye biashara wasizozielewa.
“Teknolojia imeleta fursa na changamoto zaidi. Je, chuo chetu cha biashara kinafanya utafiti ili kusaidia kuongeza tija katika fursa hizi?” ameuliza.
Ameongeza: “Bado, baadhi ya bidhaa za Tanzania hazina ubora wa kushindana katika masoko ya pamoja yanayoibukia. Utafiti wa wataalam wa biashara, hasa wakati wa mapinduzi ya teknolojia, lazima ufanyike kusaidia katika hili.’’
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, alikiagiza chuo hicho kufanya utafiti utakaoboresha bidhaa na kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema tafiti za taasisi hiyo inayojulikana kwa kuzalisha wataalam katika sekta ya biashara, zitaendelea kutumika katika kuboresha sera na mikakati ya viwanda na biashara nchini.
“Tunaitaka CBE kuendelea kutoa elimu na tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda na biashara nchini,”amesema Dk Abdallah.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tandi Lwoga, amesema tayari wameanza kutumia teknolojia mbalimbali kuwezesha vitabu na machapisho kupatikana kwa wanafunzi na umma.
Amesema CBE pia imekuwa ikitumia makongamano kukutana na wafanyabiashara hasa wajasiriamali kuwapa elimu ya mwenendo sahihi wa biashara na matumizi ya teknolojia. Tangu 2018, wajasiriamali 1,272 wamefunzwa.
“Wanafunzi wetu wanafanya utafiti katika maeneo ya kiuchumi, na tayari tumetenga karibu Sh300 milioni kwa ajili ya wahadhiri wetu kufanya utafiti katika maeneo ya teknolojia ya biashara kwa sababu ndiko tunakoelekea,” amesema.
Ameongeza: “Tumekuwa na tutaendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali hawa, hatutaki tafiti zetu ziishie maktaba ndiyo maana tumeanzisha makongamano haya ili kushirikishana matokeo na kuwasaidia wajasiriamali.’’
Amesema tangu mwaka 2020, CBE imewasilisha na kushiriki matokeo ya utafiti 334 kwa wajasiriamali, ikiona athari kubwa katika mwenendo wa biashara, uwekezaji katika viwanda na sekta ya ICT.
“Tumekuwa tukitengeneza muhtasari wa sera kutokana na tafiti hizi na kuziwasilisha kwa mamlaka husika ili zifanyiwe kazi. Pia tumeanzisha midahalo ya mtandaoni ili kutangaza matokeo ya tafiti na ufumbuzi wa changamoto za biashara,” amesema Profesa Lwoga.