Wanafunzi wenye ulemavu Kawe waomba kukarabatiwa madarasa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Kawe iliyopo Manispaa ya Kinondoni wameomba wadau kujitokeza na kukarabatia madarasa yao ili waweze kujifunza vizuri.

Shule hiyo ilikuwa na madarasa matatu ya wanafunzi 52 wenye ulemavu ambao ni wasioona, wenye ulemavu wa viungo, ulemavu wa akili, usonji na viziwi lakini kwa sasa hayatumiki kutokana na kuchakaa.

Wanafunzi hao waliwasilisha ombi hilo Julai 2,2024 kwa Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) ambayo iliwatembelea na kutoa msaada wa vyakula, vifaa tiba na vingine pamoja na kuwafanyia uchunguzi wa awali wa kiafya watoto wenye ulemavu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Wilbert Mfwangavo, amesema wamelazimika kuwapunguzia mikondo wanafunzi wasio na ulemavu ili yapatikane madarasa mawili kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu.

“Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapaswa kuwa wachache katika chumba cha darasa ili waweze kujifunza vizuri, tulikuwa na madarasa ya elimu maalumu matatu, kwa muda mrefu yametumika bila kukarabatiwa imefikia hatua yamepata nyufa nyingi na paa zinavuja. Mwaka jana wahandisi wa manispaa walipita na kushauri tusiwaweke wanafunzi katika madarasa hayo tuwahamishe mpaka tutakapoyakarabati.

“Tuliwahamisha wanafunzi na kuwapeleka katika madarasa mengine, tumehakikishiwa kwamba katika bajeti ya 2024/2025 yatakarabatiwa. Lakini tunapokutana na marafiki kama hawa (CCCC) huwa tunawaomba watusaidie kuuga mkono jitihada za serikali katika kuboresha elimu,” amesema Mwalimu.

Amesema watoto hao wanalelewa sawa na wengine kwa kuwapa kipaumbele ili waweze kujifunza vizuri ambapo pia wanashirikiana na serikali ya mtaa kuwafichua waliofichwa majumbani kuhakikisha wanapata elimu.

Kiongozi wa kundi la madaktari kutoka China, Dk. Zhang Kai, amesema wameguswa kuwafanyia uchunguzi wa awali watoto hao ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora itakayowawezesha kusoma wakati wote.

“Tuko madaktari zaidi ya 10 tunatoa huduma katika hospitali mbalimbali hapa Tanzania kama vile Muhimbili, lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika utoaji huduma za afya na kuimarisha uhusiano na urafiki uliopo baina ya nchi zetu,” amesema Dk.
Kampuni hiyo ilikabidhi vyakula, vifaa tiba, viti mwendo, mashine ya kufulia, friji kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu kwa watoto hao.

Mtendaji wa Kata ya Kawe, Husna Nondo, ameshukuru kwa msaada huo kwani utasaidia watoto hao kujifunza katika mazingira rafiki na kuinua kiwango cha elimu.

Related Posts