Tabora. Serikali imezindua mfumo wa wakulima na wafanyabiashara kujisajili kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya kitaifa ya Nanenane ambayo kitaifa mwaka huu yatafanyika jijini Dodoma.
Mfumo huo umezinduliwa leo Julai 6, 2024 mkoani Tabora na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko ikiwa ni maandalizi ya sikukuu ya wakulima nchini itakayoadhimishwa Agosti 8, 2024.
Akizungumzia mfumo huo, Dk Biteko amesema anaamini mfumo huo utakuwa wa mfano kwa kuwasaidia wafanyabiashara wanaopanga kwenda Dodoma kwenye maonyesho, maana wapo ambao walikuwa wanashindwa kushiriki kwa kukosa nafasi.
“Mkautumie mfumo huu kujiandikisha kwa wingi kuelekea maonyesho ya Nanenane ambayo nimeambiwa yatafanyika jijini Dodoma, kikubwa ni kwamba wizara imeona kuna haja ya kuendana na ukuaji kwa teknolojia na mfumo huu ukawe dawa kwa kuhakikisha tunapata wafanyabiashara na wakulima wengi ambao watajitokeza kwenye maonesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka,” amesema Dk Biteko.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mfumo huo unalenga kuwaondolea usumbufu wakulima na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilazimika kutafuta vibali wizarani kwa ajili ya kushiriki maonyesho hayo.
“Mfumo huu wa kusajili wakulima na wafanyabiashara ambao wanashiriki maonyesho ya Nanenane, umeanza kufanya kazi mwaka huu, utarahisisha washiriki wa Nanenane kujisajili bila kufunga safari kuja wizarani na hata mikoani pia, hivyo wale waliojiandaa kushiriki maonyesho ya mwaka huu waanze kujisajili ili wapate nafasi na kibali cha kufanya shughuli zao kwenye maonyesho hayo.
“Tunatambua kwamba kwa kuwa ni mara ya kwanza kuutumia mfumo huu, utakuwa na changamoto kwa watumiaji, hatutaishia hapo, bali tumejipanga kuwasaidia wote ili washiriki ipasavyo kwenye hayo maonyesho,” amesema.
Dk Biteko yuko mkoani Tabora kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani ambapo kwa mwaka huu yamefanyika mkoani hapa kwenye viwanja vya Nanenane Ipuli ambapo vyama mbalimbali vimejitokeza kufanya maonyesho.