Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya afya nchini, wametoa maoni yao wakitaka muundo rasmi uwekwe katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupambana na changamoto ya wahitimu wa kada ya afya kukosa ajira, hususani madaktari na wauguzi.
Wamesema kada hiyo ni muhimu na inahitajika zaidi nchini, kwani changamoto ya ubora wa huduma inachagizwa na uhaba wa watumishi wa afya katika vituo vya kutolea matibabu.
Akitoa maoni hayo, Profesa Abel Makubi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma (BMH), amesema lazima kuwe na mikakati ili rasilimali fedha inayowekezwa kusomesha wataalamu hao isipotee.
Profesa Makubi ametoa maoni hayo, wakati wa kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, linalofanyika leo Jumamosi, Julai 6, 2024 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere JNICC.
“Ajira ni changamoto kubwa sekta ya afya, tunao zaidi ya madaktari 3000 na wauguzi 25,000 hawana ajira, hili suala linaniogopesha sana. Lazima tuweke mikakati katika dira ijayo, hawa watu wasiendelee kuzagaa katika jamii yetu, hii ionekane kwenye dira yetu,” amesema Profesa Makubi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejikita katika maeneo sita ikiwemo maboresho ya kiuchumi, kijamii, utawala bora haki na amani, sayansi ya mabadiliko ya kidijitali, utunzaji mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.