ACT Wazalendo walivyokerwa na kauli ya Mazrui, akiri kosa wayamaliza

Unguja. Chama Cha ACT-Wazalendo kimeweka wazi jinsi viongozi na wanachama walivyokerwa na kauli ya Naibu Katibu Mkuu mstaafu, Nassor Mazrui kumsifu hadharani Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na kumtaka asisikilize maneno ya wakosoaji badala yake aendelee kuchapa kazi.

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa jana Jumapili, Julai 7, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mchangani Malindi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud na kiongozi wa chama mstaafu, Zitto Kabwe.

Hata hivyo, Jussa amesema tayari viongozi wameshakutana na Mazrui kujua kilichomsibu na yeye kukiri alikosea lakini akasema wanaosubiri aende Chama cha Mapinduzi (CCM) watasubiri sana.

Kauli inayoelezwa kuleta taharuki kwa wanachama na viongozi wa chama hicho ilitolewa Julai 1, 2024 wakati Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Afya Zanzibar alipomkaribisha Rais Mwinyi kuzungumza na wananchi alipokuwa akifungua nyumba 76 za watumishi wa afya zilizojengwa na Serikali ya China katika hospitali ya Abdallah Mzee Mkoa wa Kusini Pemba.

Katika maneno yake Mazrui alisema: “Mimi ni waziri wako umenichagua katika wizara ya afya ila nataka nikwambie kwamba huu ni mwaka wanne unatuongoza, nchi ipo katika amani na utulivu na tunakusifu kwa moyo wako wa subira na huo ndio uongozi, kiongozi lazima awe makini awe na gozi ngumu.”

“Mheshimiwa Rais endelea kutuongoza, manenomaneno hayo usisikilize kamata mstari mmoja sisi tupo nyuma yako tunafanya kazi na wewe amani na utulivu ni vyetu sote, katika uchaguzi kila mwananchi ana hiari yake, kila mwananchi anaona unayoyafanya, anaona nia yako.”

“Kwa hiyo kila mtu atatumia demokrasia yake na haki yake ya kuchagua lakini kazi unayoifanya tunaiona na naomba uendelee hivyohivyo wala usiyumbe timiza wajibu wako na sisi tupo nyuma yako tunafanya kazi kwa ajili ya Wazanzibari, hatufanyi kazi kwa ajili ya mtu yeyote,” alisema 

Katika mkutano huo, Jussa amewaeleza wanachama na wafuasi wa chama hicho kwamba kauli ile sio tu ilileta taharuki kwao pekee bali viongozi na kwamba waliokerwa na kauli hiyo walikuwa na haki kuumizwa nayo.

Kwa mujibu wa Jussa wamekaa katika kamati ya uongozi ikateua viongozi watatu: Mwenyekiti wa Taifa mstaafu, Juma Haji Duni (Babu Duni), Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara, Issiaka Mchinjika na yeye Jussa kwenda kuzungumza na Mazrui na aliwaeleza kilichomsibu.

“Lakini moja la kiungwana Mazrui alisema nataka nikiri na niwaombe radhi kwamba nimewaumiza wenzangu, akatueleza mazingira ya mkutano yalivyokuwa, lakini tukamueleza kwamba pamoja na mazingira ya mkutano wanachama na viongozi hawakuridhika na kauli hiyo,” amesema Jussa.

Kwa hiyo ametuthibitishia akisema: “Wanaongoja mkono ukatike wasahau mimi ni ACT Wazalendo na nitakufa nikiwa ACT, la pili akatuambia likitokea kama lile wachukue hatua dhidi yangu mimi nitalipokea, kwa hiyo hili tumelifunga na tumelimaliza.”

Tofauti na ilivyo kawaida kila mkutano wa hadhara wa chama hicho Mazrui anakuwapo lakini katika mkutano huo hakuwapo, hata alipotafutwa kwa njia ya simu kuhusu kukiri kosa na kutorudia, simu yake haikupokewa wala kujibu ujumbe mfupi.

Kuhusu kauli iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto kwamba chama hicho kikimfukuza wanamkaribisha Mazrui, Jussa amesema “Papa havuliwi kwa dema watakaa wasubiri sana, safu ya ACT iliyojipanga wajiandae mwakani kuondoka na ACT kuingia madarakani.”

Akikazia jambo hilo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud amesema ikiwa mtu anataka wema anatakiwa atengeneze wema badala ya kusubiri kudandia kusifiwa hadharani kwani wema haudandiwi.

“Kama wewe ni kiongozi ni jambo jepesi sana, fanya kuwatendea watu wema, hata hilo lililosemwa inaonyesha jinsi gani watu wamekosa uungwana, kwamba mtu ambaye mmempiga, mkamharibia na familia yake, mkamtia ulemavu leo kapata kuwashukuru basi nyie mnakosa kusikitika mnaandaa kuja kufanya mengine kuliko yale, waseme wenye kusema lakini wengine nyamazeni na hili tutafakari sana ndugu zangu,” amesema.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, amesema kuna kauli ambazo zimekuwa zikitolewa kwamba chama hicho kinatukana na kutoa kauli mbaya “ukiwa fisadi, ukiiba tukuiteje, unataka tukuite sheikh, imamu, kama unataka hivyo fanya ya imamu tukuite hivyo, sisi niwaambie ndugu zangu tutaendelea kuyasema haya kwa sababu ndio wajibu wetu na tunasema kwa sababu nchi yetu inatuuma na kutuumiza.”

Kwa mujibu wa Othman, CCM kinaona wivu kinapoona ACT wanafanya mikutano ya hadhara kwani wao wameshindwa kufanya mikutano yake wanadandia kwenye shughuli za Serikali, “wanabaki kusema hawa wanatukana Rais, wanatukana Serikali, lipi ambalo limetukana Serikali.”

Amesema wataendelea kusema na kuyaweka hadharani maovu ili kila mtu ayasikie mambo hayo sio ya shangazi yake mtu wala mjomba wake mtu bali hiyo nchi ni ya watu wote na kwamba wanayasema kwa sababu wanaumia maana nchi imefanywa fukara.

Othman amesema pamoja na utukufu na neema zote ilizonazo Zanzibar, haipaswi kuwa ilivyo sasa,  huku akiilinganisha nchi ya Mouritius ambayo ni ndogo kwa Zanzibar lakini katika bajeti ya mwaka huu imepitisha Sh13 trilioni kwa fedha zao za ndani kati ya fedha hizo Sh1 trilioni ndio mkopo.

Amesema ndicho wanachokipambania na wana uhakika wakipata uongozi mathubuti wenye uchungu na nchi watafanikiwa kufika huko, kwani waliofika hawakupata miujiza bali ni kupata viongozi waadilifu na Zanzibar imelikosa hilo.

“Kichaka tunakwenda kukitia moto na mti huu tunakwenda kuung’oa na ndio maana tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kura yenu ije iwaletee mageuzi yanayokubalika,”

Akilijibu hilo, Mbeto amesema  hizo ni propaganda na chama hicho hakina tena sera baada ya Serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo hivyo kuona wameshikwa pabaya.

Zitto afichua siri ya vikao

Awali, Kiongozi wa chama mstaafu, Zitto Kabwe amesema viongozi wanaoongoza chama hicho waliopo na wastaafu kazi wanayoifanya usiku na mchana bila kulala ni kuhakikisha uchaguzi mwaka 2025 unakuwa huru na haki.

Amesema hawataki kusikia mambo ya kupiga kura siku mbili: “Hatutaki kwamba watu wanapiga kura leo wengine kesho hiyo ni njia ya kutaka kuiba kura na hii ndio kazi ambayo viongozi wanaifanya na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na uimara wa viongozi wetu lazima tutakuwa na mabadiliko yanayotakiwa, tutakuwa na mfumo wa kupiga kura kwa siku moja tushinde na kuunda Serikali na mwenyezi Mungu atatusaidia.”

Zitto amesema hilo ndilo jambo kubwa linawanyima usingizi viongozi wa chama: “Hili ndilo ambalo hata vikao vyetu ambavyo tumevimaliza wikiendi hii sehemu kubwa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Mzanzibari hapotezi maisha kwa sababu ya uchaguzi, hapotezi ndugu jamaa na marafiki, hapotezi kiungo cha mwili wake.”

Zitto amesema: “Kazi ya kuhakikisha mkipiga kura zenu zinahesabiwa na anayeshinda anapewa nafasi ya kuongoza, hii ndio kazi ambayo inatusumbua muda wote, viongozi wenu wanahangaika kucha kutwa, hawataki kusikia yaliyotokea nyuma.”

Amesema Wazanzibari ni ishara muhimu ya watu ambao hawakati tamaa katika kupigania haki, demokrasia na kupigania Zanzibar moja, yenye mamlaka kamili.

Amesema chama kitaendelea kuwa pamoja nao kuhakikisha wanafikia demokrasia wanayoitaka na Zanzibar itakayoweza kujiamulia mambo yake na wananchi wake wanaishi kwenye uchumi unaokua.

Amefafanua kuwa chama hicho kinatambua madhila, vipigo na mauaji ambayo Wazanzibari wameyapitia katika nyakati zote za kupigania haki na demokrasia.

“Mauaji haya, vipigo hivyo ndio mambo kila siku tukiamka asubuhi yanatupa morali kuendelea kupigania haki na demokrasia kwani siku tukiacha mapigano haya tutakuwa tumewasaliti waliomwaga damu kwa ajili yetu, na mwenyezi Mungu hatatusamehe na tutakuwa tumemsaliti mzee wetu Maalim Seif Sharif Hamad,” amesema Zitto.

Related Posts