Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuondoa vikwazo na kusitisha mara moja mipango na operesheni za kuwaondoa wamachinga eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam na maeneo mengine mijini.
Chama hicho kimetoa kauli hiyo kwa maelezo kuwa kina wasiwasi kutokana na madai ya wafanyabishara wa Kariakoo katika mgomo wa hivi karibuni kuwataja wamachinga ni kero na kikwazo katika biashara zao.
Taarifa iliyotewa jana Jumapili, Julai 7, 2024 na Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara ACT-Wazalendo, Mwanaisha Mndeme, imeeleza kuwa hatua hiyo ni kuwatoa kafara wamachinga na kuwaweka katika hatari zaidi ya kuondolewa kwa nguvu na kunyimwa haki ya kutumia miji na majiji kujipatia kipato.
“Ni wazi sasa Serikali inaenda kutekeleza kwa nguvu zote baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuliagiza Jeshi la Polisi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na biashara kuwapanga wamachinga eneo la Kariakoo na maeneo mengine chini.”
Chama hicho kimeenda mbali zaidi na kupinga vikali kile ilichokiita baraka za Rais kwa kuwa uhalisia na uzoefu unaonyesha kinachokwenda kutekelezwa ni kuondolewa katika maeneo yao ya asili ya kibiashara.
“Kauli hii ni tangazo la operesheni ya fukuzafukuza ya wamachinga ambayo kwa miaka yote inaishia kuwaumiza, kuwafukarisha na kuleta hasara kubwa kwa wananchi hawa,” kimesema chama hicho.
Aidha, kimehoji iwapo Serikali imekataa kabisa kujifunza katika operesheni zote ilizoziendesha kuwa na mtazamo mpya wa namna miji inavyopaswa kuwa, ili kuakisi mahitaji ya jamii tuliyonayo leo na tunayotamani kuijenga.
“Serikali haitaki kuangalia upya mipango ya miji na matumizi ya maeneo yote ya wazi, ili kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara na ustawi wa wamachinga nchini?” kimehoji.
Hata hivyo, chama hicho kimesema kitaendelea kuhakikisha kinazuia ukandamizaji, kuhamishwa na kuondolewa kwa wamachinga mijini na katika masoko yao ya asili kama vile maeneo yenye mzunguko mkubwa wa watu.
“Tunawasihi wamachinga kuwa na umoja na mshikamano katika wakati huu mgumu ambao Serikali imekusudia kuwaondoa kwenye maeneo yao ya biashara.
“Tunaungana na wafanyabiashara wadogo nchini katika kipindi hiki cha sherehe za Sabasaba kupigania mazingira rafiki ya kibiashara, ili kutumia maeneo mbalimbali ya miji kujipatia kipato na kuinua maisha yao,” imeeeleza taarifa hiyo.
Msingi wa kauli ya ACT unatokana na kile ilichokisema wamachinga wamekuwa waathirika wakubwa wa mipango ya Serikali kila inapojaribu kushughulikia matatizo ya wafanyabiashara nchini Tanzania.