AZAM inafanya mambo kimyakimya kwani tayari ilishatangulia kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya kabla ya kesho kwenda Zanzibar kuendeleza kambi hiyo na baadae kupaa hadi Morocco na ikirudi nchini itakuwa na kazi ya kusaka mataji katika michuano ya msimu wa 2024-2025.
Awali Azam ilikuwa iondoke Dar es Salaam leo, lakini ikasogeza mbele hadi kesho itatua Zanzibar kwa kambi ya siku tano.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Azam, Thabit Zakaria ‘Zakazi’ ameliambia Mwanaspoti, wakiwa Zenji mbali na mazoezi, lakini ratiba ya kikosi hicho itahusisha mchezo mmoja wa kirafiki.
“Timu itaondoka Jumanne, tumesogeza mbele kwa sababu za ndani ya klabu, Zanzibar tutakuwa huko hadi Julai 13 kuwahiratiba nyingine za safari,” alisema Zaka.
Azam ikirejea tu, Julai 14 itapaa kwenda Morocco kuendeleza maandalizi kwa siku 16 hadi Julai 30 kisha kurejea nchini kujindaa na mechi za Ngao ya Jamii ikitarajiwa kuanza na Coastal Union.
“Tukiwa Morocco tunaweza kucheza mechi tatu za kirafiki kulingana na ratiba ya makocha, baada ya siku 16 tutarudi nchini kuendelea na ratiba nyingine. Kitu muhimu ni kwamba mazoezi tuliyoayoanza hadi sasa makocha wanafurahishwa na utayari wa wachezaji na umakini ni mkubwa, licha ya ratiba ya mazoezi ngumu,” alisema Zakazi na kuongeza;
“Tuna malengo makubwa msimu ujao, kuhakikisha tunapata mataji ya ndani, ila kufika angalau makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndo maana mnaona aina ya usajili mkubwa tulioufanya.”
Azam imesajili nyota wanane wapya washambuliaji Nassor Saadun, Adam Adam, Jhonier Blanco, viungo Ever Meza, Franck Tiesse na beki Yoro Diaby.