Beki Yanga asaini mmoja Simba

BEKI wa kushoto wa Yanga Princess, Wincate Kaari amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Simba Queens kwa msimu ujao.

Kaari anakuwa mchezaji wa tatu kutoka Yanga Princess kujiunga na watani zao, Simba Queens, katika dirisha hili la usajili baada ya awali Precious Christopher na Saiki Atinuke kupewa kandarasi ya kuitumikia timu hiyo.

Habari za ndani kutoka klabuni hapo zilieleza kuwa beki huyo Mkenya aliandika barua ya kuondoka klabuni hapo akidai anahitaji kupata changamoto mpya ambayo tayari amepewa mkataba wa mwaka mmoja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msimamizi wa mchezaji huyo alisema ni kweli beki huyo amehamia Simba akiwa huru baada ya mkataba wake kutamatika.

“Mchezaji mwenyewe aliniambia akimaliza mkataba hataongeza ingawa Yanga nao tulikaa nao na kuzungumza lakini tayari tulikuwa na ofa mbili za ndani na mbili kutoka nje,” Alisema kiongozi huyo na kkuongeza

“Nilipozungumza na mteja wangu akasema anataka kucheza kutokana na malengo yake ya kufika mbali,  ikumbukwe Simba itawakilisha Tanzania kwenye mashindano ya CECAFA ndio tunakubali kusaini na muda wowote atatambulishwa.”

Alipotafutwa Meneja wa Simba, Selemani Makanya alisema “Tukimaliza kusajili kila mmoja atajua sasa hivi tupo mawindoni.”

Related Posts