Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewataka watoa huduma za afya nchini kutimiza majukumu yao, ikiwamo kuwa na lugha nzuri kwa wananchi wanaokwenda kupata matibabu katika hospitali, zahanati au vituo vya afya.
Kimesema hakitakuwa na maana kuwepo na majengo mazuri ya hospitali au vifaa tiba vya kisasa, huku mapokezi na huduma kwa wagonjwa hazirishishwi.
“Unajua muda mwingine hata lugha ya kumpokea mgonjwa anapona, lakini ukimpokea na kumwambia kuna kila kitu, halafu lugha yako siyo nzuri unamkatisha tamaa,” amesema Amos Makalla Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.
Makalla ametoa wito huo leo Jumatatu Julai 8, 2024 alipotembelea kituo kipya cha afya cha Kinyerezi, jijini Dar es Salaam kilichopandishwa hadhi kutoka zahanati.
Kituo cha Kinyerezi kinatajwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo mengine jirani na Wilaya ya Ubungo, waliokuwa wakifuata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Amana, jijini Dar es Salaam.
“Mtu anapokuja hapa (hospitali) ana shida anahitaji lugha ya kumpa matumaini, ndiyo kiapo mlichoapa. Kituo hiki kitakuwa na maana na watu kukimbilia kutokana na huduma bora,” amesema Makalla
Jana Jumapili Julai 7, 2024 akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Chanika, Makalla alipokea kero za huduma za matibabu katika kituo cha afya cha Nguvu kazi kwa wajawazito.
Kutokana na hilo, Makalla aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, alimuagiza mganga mkuu wa wilaya ya Ilala, Dk Zaituni Hamza kuitatua changamoto hiyo haraka.
Katika hatua nyingine, Makalla amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za jamii, ili kuleta maendeleo kwa wananchi kwa vitendo zaidi akisema haihataji kutumia tochi kumulika.
Amesema kituo cha afya cha Kinyerezi kina majengo ya kisasa na vifaa vya tiba vya kutoa huduma mbalimbali, akisema ikitokea mtu anakwenda Amana au Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, basi ana tatizo kubwa linalomsibu.
“Hapa kuna huduma na vipimo vya kisasa vya hali ya juu vya magonjwa yote na operesheni ndogo ndogo, kuna wodi za wazazi za kisasa kabisa,” amesema Makalla.
Kwa upande wake, Dk Hamza amesema kituo hicho kinahudumia zaidi ya wagonjwa 200, 000 kutoka mitaa ya sita ya Kinyerezi sambamba na kata jirani za Bonyokwa, Gongo la Mboto, Kifuru na Mbezi Luis ya wilayani Ubungo.
“Awali kwa siku wajawazito watatu hadi wanne walikuwa wakijufungua, sasa hivi ni 15 hadi 17 kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kituo hiki,” amesema Dk Hamza.
Awali, Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alitembea ujenzi wa shule ya kisasa ya sekondari ya ghorofa Minazi Mirefu, akisema ameridhishwa na mchakato huo utakaogharimu zaidi ya Sh1bilioni.