DAWASA yatekeleza agizo la waziri ndani ya siku 3

KAIMU Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire amesema mamlaka hiyo imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji, Jumaa Aweso la kufanya maunganisho ya majisafi kwa wananchi wa maeneo ya Kigamboni kwa kutoa vifaa vya maunganisho ya majisafi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Amesema hayo katika hafla ya kukabidhi vifaa vya maunganisho mapya kwa wananchi 45 vilivyokabidhiwa kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ofisi za DAWASA Kigamboni ikiwa ni jitihada za kuchagiza utekelezaji wa mpango wa utoaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi.


Ameeleza kuwa hii ni hatua ya awali ambapo wateja 45 waliokwisha kulipia wataungiwa ndani ya siku mbili.

Amesema kazi inaendelea ya kuwaunganisha wateja wengine 400 ambao wameshapewa makadirio ya gharama ya maunganisho kulipa ili waweze kuunganishiwa na kunufaika na huduma ya majisafi.

Sambamba na hiyo amewataka wananchi kuleta maombi ya kupata majisafi ili waweze kufanyiwa upimaji na waweze kunufaika na huduma hii muhimu.

Kwa upande wake Katibu wa CCM, Stanley Mkandawile ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuitikia kilio cha wananchi kuhusu huduma ya maji kwa kutoa vifaa vya kuwaunganisha wateja na majisafi.

Mmoja wa wanufaika wa zoezi la maunganisho mapya, Yusufu Msabila naye ameishukuru DAWASA kwa kumfungia maji nyumbani kwake na sasa anaanza kunufaika na huduma.

Related Posts