Jela miaka minne kwa kumjeruhi mama yake mdogo

Geita. Mahakama ya Wilaya ya Chato imemuhukumu kifungo cha miaka minne na kulipa faini ya Sh3 milioni, Faida Enock mkazi wa Bwanga, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumjeruhi Monica Laurent kwa kumkata na kitu chenye ncha kali na kusababisha kuondolewa kwa vidole vyake vinane vya mikono.

Hukumu hiyo ilitolewa Julai 5,2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Erick Kagimbo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo akiwa na nia ovu.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mauzi Lyawatwa ameieleza Mahakama kuwa Julai 20,2022 saa mbili usiku, mshtakiwa alimshambulia Monica ambaye ni mama yake mdogo akiwa nje akiandaa chakula cha usiku na kumsababishia majeraha katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Katika kesi hiyo namba 757/202 ilielezwa kuwa baada ya mshtakiwa kutekeleza unyama huo aliondoka na kwenda kujificha kabla ya kukamatwa na Polisi.

Mshtakiwa huyo alidaiwa kutenda kosa la kujeruhi mtu mwingine kinyume na kifungu cha 225 cha Sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kufuatia kutiwa hatiani Wakili wa Jamhuri uliiomba Mahakama hiyo kutenda haki kwa kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine kwani kitendo kilichofanywa kimemuacha Monica na ulemavu wa kudumu na kubaki kuwa tegemezi.

Akijitetea mahakamani hapo, Enock ameiomba Mahakama kumuonea huruma na kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana watoto wadogo wanaomtegemea,  pamoja na mama yake mzazi ambaye ni mlemavu aliyekua akiishi naye.

Kufuatia ungamo hilo, Hakimu Kagimbo alimuhukumu kwenda jela miaka minne na kulipa fidia ya Sh3 milioni ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Hata hivyo, ameeleza mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa endapo hajaridhika na adhabu iliyotolewa.

Related Posts