JKT Tanzania imemuajiri Jemadari Said Kazumari kuwa mtendaji mkuu na imeelezwa ndiye anayesimamia usajili unaofanywa kwa ajili ya msimu ujao, huku mojawapo wa usajili aliofanya ni kumshawishi John Bocco kujiunga na timu hiyo.
Mwanaspoti imepata taarifa za ndani kwamba umebaki utambulisho wa Kazumari, lakini tayari ameishaanza kuyafanya baadhi ya majukumu yake kujua timu itaweka wapi kambi.
“Uongozi umepanga kufanya utambulisho wa pamoja kwa maana ya wachezaji, benchi la ufundi na Kazumari, hivyo ni suala la muda, kama unavyojua kila kitu kina utaratibu wake hasa jeshini,” amesema mmoja wa mabosi wa timu hiyo.
Kazi ambayo atakuwa nayo Kazumari ni kufanya uamuzi mkubwa wa timu, kuendesha mwelekeo wa timu, kusimamia watendaji wengine, kusimamia mipango ya ukuaji, kuwajibika kwa bodi ya wakurugenzi na anakuwa sura ya timu.
“Ujio wake utaongeza kitu kwenye timu, kwani ana uzoefu mkubwa kwenye soka, ukiacha kucheza kwake kwa mafanikio pia amewahi kuongoza moja ya timu hapa nchini,” amesema.
WASIFU WAKE
Kazumari siyo mgeni katika masuala ya uongozi kwani aliwahi kuwa meneja wa Azam FC, ofisa maendeleo na mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Pia ni mchezaji wa zamani wa Kariakoo Lindi, Mukura Victory ya Rwanda, 82 Rangers na Kahama United zote za Shinyanga, Vijana ya Ilala na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Ukiachana na hilo ni ana taaluma ya ukocha (Diploma B) na anawasimamia baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara.
JKT Tanzania imeingia kambini juzi Jumamosi, ambapo itakaa jijini Dar es Salaam wiki mbili na mbili nyingine itakwenda jijini Mbeya.