BAADA ya mawindo ya muda mrefu, Yanga imefanikiwa kupata saini ya kiungo Mzambia Clatous Chama kutoka Simba na tayari imemtambulisha. Ilikuwa ndoto ya Wanajangwani kumpata staa huyo na sasa imetimia huku kibano kikigeukia kwa Simba na nyota wa Azam, Feisal Salum maarufu Fei Toto.
Kabla ya kutua Yanga, Chama aliumiza sana vichwa vya viongozi wa timu hiyo. Walimhitaji tangu mwaka 2019 baada ya kuanza vyema Simba aliposainiwa mwaka 2018 lakini walimkosa.
Karibu kila dirisha la usajili, Yanga ilifanya jaribio la kupata saini ya Chama lakini haikufanikiwa. Ilifika sehemu mashabiki wa Simba wakawa wanawatania wenzao wa Yanga; “Mnamsajili kila msimu lakini ligi ikianza anacheza Simba…”
Sasa imekua. Chama ni Mwananchi baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezwa wa pili akifanya vyema. Mashabiki wanasubiri kumuona akiwa ndani ya jezi za kijani na njano. Hilo litatimia siku chache zijazo.
Baada ya Yanga kumpata Chama, kibano kimegeukia kwa Simba na Fei Toto. Unajua kwanini? Endelea kusoma.
Simba inahitaji saini ya Fei Toto lakini kwa namna hali ilivyo dili hilo kwa sasa haliwezi kukamilika.
Mwanaspoti linajua, Simba inamtaka Fei Toto lakini Azam haiko tayari kumuachia kwa sasa. Inaelezwa awali baadhi ya viongozi wa Azam walitaka kumuweka sokoni Fei Toto kwa dau la Sh1.3 bilioni lakini ‘mwenye timu yake’ akagoma.
Mwenye timu yake anayezungumziwa hapa ni tajiri Yusuf Bakhresa. Huyu ndiye roho ya Azam kwa sasa kama ilivyo kwa Simba na Mohammed Dewji ‘Mo’ au Yanga na Gharib Said ‘GSM’.
Yusuf ndiye anatoa mkwanja pale Azam na ndiye anakamilisha sajili nyingi ikiwemo ile tata ya Fei Toto kuikacha Yanga na kutua Azam na sasa amegoma Fei Toto kuuzwa kwa gharama yeyote.
Tajiri huyo anaamini Fei Toto ni nguzo ya timu hiyo katika kufika malengo hivyo kwa sasa hauzwi, labda baadaye.
Achana na Yusuf. Tutamzungumzia siku nyingine. Turudi kwa Fei Toto na Simba.
Kama ilivyokuwa kwa Yanga na Chama ndivyo ilivyo kwa Simba na Fei Toto. Simba inamtaka Fei Toto karibu kila msimu lakini haimpati. Lini itampata? Hatujui.
Nakurudisha nyuma mwaka 2018. Fei Toto akiwa ‘Bwana Mdogo’ ndani ya kikosi cha JKU kwenye michuano ya Mapinduzi Cup aliuwasha moto sana.
Simba na Yanga zikaingia vitani kutaka saini ya Fei Toto. Zote zikazidiwa ujanja na Singida United iliyomsainisha mkataba wa miaka miwili.
Simba ikakata tamaa na kukubali yaishe. Yanga ikaendelea kukomaa na Julai 12 2018 ikatokea kituko cha kufurahisha na kuhuzunisha kwa wakati mmoja.
Siku hiyo mchana, Fei Toto alitambulishwa kama mchezaji wa Singida United, lakini jioni akatambulishwa kama nyota mpya wa Yanga.
Mashabiki wa Yanga walifurahi. Wale wa Simba walihuzunika na kustaajabu imekuwaje, lakini baadaye ilifahamika ni umafia umefanywa na aliyekuwa kiongozi wa juu wa Singida ambaye ni shabiki kindakindaki wa Yanga ndiye aliyesimamia shoo hiyo. Ikaisha hivyo.
Jioni hiyo Feisal akatambulishwa Yanga akifuatana na Jaffar Mohamed aliyesainiwa akitokea majimaji. Wino ulimwagwa chini ya Hussein Nyika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga kwa wakati huo na Fei Toto akawa Mwananchi kwa mkataba wa miaka mitatu. Simba ikatoka patupu.
Muda ukaenda, ikawa kila msimu Simba inaongea na Fei Toto ikitaka kumsajili. Ikawa inashindikana. Fei Toto akaendelea kubonda mali Yanga. Timu hiyo ikapitia kipindi kigumu. Simba ikataka kutumia njia hiyo kumnyakua Fei Toto lakini ikashindwa tena.
Ikawa hivyo karibu kila dirisha la usajili lakini Fei Toto akasalia kucheza Yanga. Mwishoni mwa mwaka jana, Fei Toto akaanzisha balaa ndani ya Yanga. Akataka kundoka na kweli akaondoka.
Viongozi wakahamaki. Anaondokaje wakati bado ana mkataba na kila kitu anapewa? Fei Toto akawa haambiwi wala haambiliki kuhusu kurejea Yanga. Kesi ikarindima TFF, Mwanaspoti ikawa inakupa kila kinachoendelea ikiwamo kukudokeza kuwa staa huyo anapewa jeuri na Azam chini ya tajiri Yusuf.
Kesi ikawa ngumu kwa Fei Toto, lakini akagoma kurudi Yanga akaendelea kula maisha mtaani hadi pale Rais Samia Suluhu alipoingilia kati na kusema Yanga na mchezaji huyo wakae wayamalize kiungwana.
Yanga ikatii amri. Ikamuuza rasmi Fei Toto kwa Azam, kijana akaenda anakokutaka. Wakati hilo halijapoa Simba ikamuhitaji Fei Toto akiwa hajacheza hata mechi moja ya Azam. Matajiri hao wa Chamazi wakagoma kumuuza.
Duru hii Simba imerejea tena Azam kuitaka saini ya Fei Toto lakini dili limeshindikana. Hatujui lini Simba itafanikiwa kumpata Fei Toto lakini huenda siku zijazo ikafanikiwa kama Yanga ilivyomnasa Chama iliyehangaika naye miaka mingi nyuma. Muda una majibu sahihi. Tusubiri tuone!