* Wakufunzi wa ufundi wapewa mafunzo ya namna ya kutengeneza majiko sanifu ya kupikia
SHIRIKA Lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organisation (KTO,) limebeba ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani gesi kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 (FDC’s) vilivyopo nchini kote kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu pamoja ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kuepukana na athari zitokanazo na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ikiwemo vifo na magonjwa ikiwemo saratani.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mafunzo maalumu ya namna ya kutengeneza majiko sanifu kwa gharama nafuu yaliyofanyika katika Taasisi ya TaTEDO leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa amesema; Mafunzo hayo ya siku sita yamehusisha wakufunzi wa ufundi kutoka Kanda saba za Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) ambao kupitia wao wananchi waliopo katika maeneo ya Vyuo watapata fursa ya kujifunza namna bora ya kutengeneza majiko sanifu yanayotumia kuni chache kwa gharama nafuu na kupunguza kasi ya uchafuzi wa mazingira.
Mjengwa amesema, KTO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s,) 54 na kwa kuangalia agenda ya Serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia wameona washiriki kwa vitendo ajenda hiyo muhimu kwa mustakabali wa Taifa.
“Katika kufikia malengo hayo kutoka asilimia 10 pekee iliyopo sasa ya watanzania wanaotumia nishati safi, Tunahitaji kwa pamoja kuunga mkono ajenda hii kwa kuhakikisha malengo haya yanafikiwa, Sisi kama wadau tuna sehemu ya mchango kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi….kutokana na uwingi wa vyuo hivi tumeangalia Kanda ambazo 7 ambazo wakufunzi wa ufundi kutoka kanda hizo wamefika kupata mafunzo haya ya namna ya kujenga majiko sanifu ya kuni ya gharama nafuu, yanayotumia kuni chache na tunategemea wakufunzi hawa watatoa elimu ya kutengeneza majiko hayo ambayo pia itapunguza matumizi ya nishati isiyo safi.” Amesema.
Aidha ameeleza kuwa katika kutimiza ajenda hiyo si kila mwananchi ana uwezo wa kutumia gesi au umeme hivyo wameona ni vyema kugusa wananchi wanaotumia nishati ya kuni katika kupika wawe na majiko ya gharama nafuu na yanayotumia kuni chache ili pia kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kulinda afya.
Amesema, Wadau wa Maendeleo wakiwemo Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA,) wameona umuhimu wa suala hilo la kuunga mkono ajenda hiyo na jitihada zinazofanywa na TaTEDO zinapaswa kuungwa mkono na KTO wameleta wakufunzi wa ufundi kutoka Kanda saba kupata mafunzo hayo kisha kuyapeleka kwa jamii maeneo mbalimbali nchini hususani vijijini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania (TaTEDO,) Estomih Sawe amesema Taasisi hiyo inahusika na uendelezaji huduma za nishati endelevu na mpango mkakati uliowekwa na Serikali wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia suala kubwa ni kuhakikisha kuna mipango na programu sahihi, rasilimali fedha na Taasisi zinazohusika kujengewa uwezo kwa ajili ya kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kikamilifu.
Ameeleza kuwa, ni vyema wadau wa ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijiji, Taasisi zisizo za Kiserikali kama TaTEDO na wajasiriamali wakashirikishwa kikamilifu katika kufanikisha lengo hilo muhimu la Serikali.
Amesema, Moja ya kazi zao kubwa katika kuunga mkono mpango huo ni pamoja na kutoa huduma wezeshi ikiwemo uhamasishaji kwa wananchi kufahamu dhana nzima ya nishati safi, kutoa mafunzo kwa Taasisi na wadau mbalimbali ikiwemo namna ya kutengeneza majiko sanifu ya kupikia kwa kuni au mkaa na kufundisha namna ya kutumia majiko sanifu ya umeme.
Sawe amesema, TaTEDO ni Shirika lisilo la kiserikali lenye malengo ya kuboresha maisha ya watanzania kwa kuchangia upatikanaji wa nishati endelevu zilizoboreshwa, kutengeneza ajira na ongezeko la kipato ili kupambana na umasikini na wamekuwa wakipambana kuisaidia Serikali katika kufanya tafiti ili kuwa na teknolojia iliyo rafiki kwa utunzaji wa mazingira.
Mapema Mei mwaka huu KTO ilizindua Kampeni ya utunzaji wa mazingira ‘Pika Kijanja, Okoa Mazingira’ ambayo pia ipo katika mpango mkakati wao wa miaka mitano 2022/2027 na pia kuwa sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliyeonesha njia na kuwa kinara katika kuhakikisha kila mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia.
Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo hayo na kueleza kuwa; Mafunzo hayo ya siku sita yamehusisha wakufunzi wa ufundi kutoka Kanda saba za Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) ambao kupitia wao wananchi waliopo katika maeneo ya Vyuo watapata fursa ya kujifunza namna bora ya kutengeneza majiko sanifu yanayotumia kuni chache kwa gharama nafuu na kupunguza kasi ya uchafuzi wa mazingira. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania (TaTEDO,) Estomih Sawe akitoa Mada wakati wa mafunzo hayo. Sawe amesema kufikia asilimia 80 ya watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia 2034 ni vyema wadau wa ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijiji, Taasisi zisizo za Kiserikali kama TaTEDO na wajasiriamali wakashirikishwa kikamilifu katika kufanikisha lengo hilo muhimu la Serikali. Leo jijini Dar es Salaam.