WAKATI Simba ikitarajiwa kupaa jioni ya leo kuelekea Misri kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa 2024-2025, beki Lameck Lawi yupo zake Dar es Salaam na kikosi cha Coastal Union akijifua tayari kwa michuano ya Kagame huku mwenyewe akisema yeye ni mchezaji wa Coastal Union.
Lawi ambaye alikuwa wa kwanza kutambulishwa ndani ya Simba kwa mastaa wao wapya kuelekea msimu ujao, inaelezwa dili hilo limekufa kutokana na kukiukwa utaratibu wa usajili wake.
Mwanaspoti lilikuwa gazeti la kwanza kuandika taarifa za beki huyo kusajiliwa na Simba kwa dau la Sh. 230m kwa mkataba wa miaka mitatu lakini mambo yakaenda tofauti baada ya pande mbili kushindwa kuelewana mwishoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lawi alisema ni kweli yupo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kambi kujiandaa na michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kesho Jumanne.
“Ndio nipo Dar es Salaam na Coastal Union kwa sababu ni mchezaji wa hii timu, tumekuja hapa kwa ajili ya kambi tunajiandaa na michuano ya Kagame,” alisema Lawi.
Rafiki wa karibu wa Lameck Lawi amelithibitishia Mwanaspoti kuwa beki huyo wa kati ni kweli alisaini mkataba wa awali wa miaka mitatu ambao uliitaka Simba kuingiza fedha kwenye akaunti ya Coastal Union Mei 31 mwaka huu lakini timu hiyo haikufanya hivyo.
“Lawi ni kweli kasaini mkataba Simba lakini ni wa awali na makubaliano yalikuwa Simba kukamilisha fedha ya usajili huo Mei 31 lakini hawakufanya hivyo, kwa upande wa mchezaji makubaliano ilikuwa ni kumuingizia Sh.130m lakini wao wameweka Sh.50m,” alisema rafiki yake huyo na kuongeza;
“Baada ya kubaini Simba wamefanya hivyo kinyume na makubaliano klabu yake ya Coastal Union imemtaka mchezaji arudishe kiasi hicho cha fedha ili waendelee na mambo mengine ikiwa ni pamoja na kusitisha biashara hiyo kufanyika.”
Rafiki huyo wa Lawi alisema makubaliano kati ya pande mbili kwa maana ya mchezaji na Simba yalikuwa ni Lawi aingiziwe fedha zake zote ndani ya muda wa makubaliano lakini biashara imekwenda tofauti na makubaliano hivyo suala la kutambulishwa kwake ni batili kwani dili halikukamilika.
“Imetushtua kuona mchezaji anatambulishwa wakati biashara haikukamilika na fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya mchezaji zimerudishwa inakuwaje viongozi wa timu hiyo wanaamua kufanya kitu ambacho sio sawa.” alihoji.
Mtu huyo alisema hakuna kitu chochote kimefanyika baina ya Lawi na Simba tangu walipokutana naye na kusaini mkataba wa awali ambao ndio ulikuwa na makubaliano hayo.