Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema wamewasilisha mapendekezo kwa Wizara ya Uchukuzi, ili wapatiwe behewa moja katika treni ya kisasa ya SGR kwa ajili ya kuendeshea na kutoa huduma za kimahakama ili kuwafikia wananchi na kurahisisha utoaji wa haki nchini.
Profesa Gabriel amesema hayo, leo Jumatatu Julai 4, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu historia na muundo wa mahakama nchini, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJA) Temeke.
‘’Mahakama imeshapeleka michoro na tayari imekubalika na kupitishwa, hivyo tunaamini tutakuwa na behewa moja la Mahakama ndani ya treni ya kisasa,” amesema Profesa Gabriel na kuongeza kuwa hatua hiyo ni kutokana na uhitaji uliopo wa utoaji haki kwa jamii.
Amesema “Shughuli za kiuchumi zinapoongezeka na uhalifu unaongezeka, hivyo kusababisha wingi wa mashauri mahakamani. Tutatumia treni hiyo kama ilivyo kwa Mahakama inayotembea.”
Kadhalika, amesema Mahakama hiyo inayotembea ndani ya treni itatoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambako itakuwepo kwa siku moja kusikiliza mashauri na siku inayofuata itakwenda kituo kingine hadi itakapoishia.
Usafiri wa treni ya kisasa ya SGR, ulianza safari zake za kawaida Juni 14, 2024, kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Akiendelea kutoa taarifa ya muundo wa Mahakama, amesema wanatarajia kupokea magari manne yatakayotumika kama Mahakama inayotembea katika mikoa mbalimbali.
‘’Kwa sasa tuna magari haya mawili ambayo hufanya kazi katika maeneo mbalimbali, lengo ni kuwafikia wananchi kwa karibu na kupunguza wingi wa mashauri,’’ amesisitiza.
Amesema Mahakama hiyo inaendelea na ujenzi wa vituo jumuishi tisa katika mikoa mbalimbali ambavyo vinatarajiwa kukamilika mwakani, ikiwemo kituo jumuishi kitakachojengwa Pemba kwa gharama ya Sh9 bilioni na kinatarajiwa kukamilika Februari 2025.
“Mpaka sasa Tanzania ina vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita ambavyo vilizinduliwa mwaka 2021 na Raisi Samia Suluhu Hassan na vimeanza kutoa huduma. Vitu hivyo vimegharimu Sh51.45bilioni hadi kukamilika.
‘’Kwa kuzingatia wingi wa watu na mashauri husika, tumeamua kujenga kituo jumuishi huko Pemba, Zanzibar ambacho kitakamilika Februari 23, 2025 na kitagharimu Sh9.8 bilioni na miundombinu hii itasaidia kupunguza wingi wa mashauri mahakamani,’’ ameongeza.
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke:
Pamoja na mambo mengine, Profesa Gabriel amesema Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke ni kituo cha kwanza Afrika, ambacho kinatoa huduma za kiwango cha kimataifa.
“Kama mlikuwa hamjui, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, ni kituo cha kwanza Afrika na cha pili duniani ambacho kinatoa huduma zake kwa kiwango cha kimataifa. Kituo hiki kimekuwa msaada kwa watu wengi, kwani mpaka sasa hupokea takribani watu 1,000 kwa siku wenye changamoto mbalimbali za masuala ya kifamilia,’’ amesema.
Amebainisha kuwa Mahakama hiyo imeboresha matumishi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambapo mifumo 19 imesimikwa, ikiwemo ya matumizi ya akili mnemba (AI) katika kutafsiri na pia imekuwa na mfumo wa kuendesha mashauri kwa njia ya mtandao.