Iringa. Huenda maisha ya ustaafu ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Lain Kamendu yakaanza kwa msukosuko, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza arudishwe kujibu tuhuma za ubadhirifu.
Kamendu aliyestaafu utumishi wa umma, Juni 22, mwaka huu, anatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa Bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lugalo mkoani Iringa.
Pamoja naye, Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Sigachuma amesimamishwa kazi, kupisha uchunguzi kuhusu ubadhirifu huo, huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ikitakiwa kuharakisha uchunguzi.
Hilo linaweza kuwa ni moja kati ya matukio mengi ya upigaji fedha yanayofanyika katika halmashauri na serikalini kwa ujumla na Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby aliwahi kueleza juu ya kukithiri kwa vitendo hivyo.
“Wapigaji ni wengi, wengine utasikia tu, mama anaupiga mwingi, sio anaupiga mwingi kwamba anamsifia kwenye moyo, anaupiga mwingi yeye anaiba fedha. Anatandika fedha halafu akija huku anajifanya anasifia,” alisema Shabiby Juni 21, mwaka huu alipokuwa akichangia Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2024/25.
Kama hiyo haitoshi, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha unaoishia 2023, ilibainisha halmashauri nchini zimeshindwa kukusanya Sh61.15 bilioni kutoka vyanzo muhimu.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Julai 8, 2024, alipozungumza na wananchi wa Kilolo mkoani Iringa, baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo, aliyosema hakufurahishwa na maendeleo yake.
Majaliwa amesema bwalo la shule hiyo halijakamilika ilhali Serikali ilitoa Sh774 milioni na Sh341 milioni zimetumika huku Sh433 milioni hazijulikani zilipo.
“Taarifa za hapa hazijanifurahisha. Serikali tumeleta fedha zote Sh3 bilioni kwa ajili ya kujenga majengo yote yaliyoainishwa kwenye ujenzi huu likiwemo jengo la utawala, mabweni , madarasa, chumba za huduma za afya, maabara na nyumba za walimu,” amesema.
Amesema ilitakiwa ujenzi huo usimamiwe na uende kwa wakati lakini haujakamilika ikiwamo bwalo hilo, jambo ambalo amedai hawawezi kuwaacha wanafunzi wale wima.
Waziri Mkuu amesema kwenye jengo la utawala, fundi madirisha hajaweka nyavu, amemaliza kazi na kwamba tayari amelipwa fedha yote.
“Lazima leo atafutwe yule fundi aletwe hapa aweke nyavu kwenye lile jengo la utawala. Amemaliza kazi, amekabidhi na hajaweka nyavu, atakuja kuweka lini? Lazima aletwe hapa. Mkuu wa Wilaya simamia hili, mhandisi ambaye ameshindwa kusimamia haya nitaelekeza baadaye,” amesema.
Amesema amekagua ujenzi wa madarasa, mjenzi amefanya ujanja wa kuhamisha madawati mabovu na kuyaficha huku darasani yakibaki mazima.
“Madawati yale yaliyochanikachanika, kiti mguu mmoja mfupi mmoja mrefu haikubaliki, hii ni fedha ya wananchi lazima thamani yake ionekane. Nimeagiza aitwe aliyetengeneza madawati na roli lake kwa gharama yake aende akatengeneze upya atuletee madawati yetu safi,” amesema Majaliwa.
Akizungumzia jengo la maabara, amesema kuna mifuniko inayopitisha maji, nyaya za umeme, bomba za gesi lakini badala ya kutengeneza vizuri, wamepachika tofali jambo ambalo litawafanya walimu kushindwa kufanya kazi yao.
“Mwalimu akigundua gesi inavuja mahali atatoaje lile tofali na nyie mmegandamiza hakuna hata mahali pa kuingiza kidole. Mtataka kumpa kazi nani? maana yake waje wabomoe, wafuatilie gesi inatoka wapi. Ondoa yale yote na tengeneza upya,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza mkurugenzi ambaye amestaafu arudishwe kuja kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, Mhandisi kusimamishwa kazi ili wapelekwe mahakamani na kueleza Sh774 milioni zimetumikaje.
“Mhandisi akae pembeni hadi uchunguzi tujue nani ni nani na yeyote aliyeingia ndani tutamchukua popote alipo,” amesema.
Ameagiza wote waliohusika kusimamishwa kazi ili uchunguzi ufanyike.
“Tunapokuta haya madudedude lazima tuchukue hatua,” amesema Majaliwa.
Akizungumzia ujenzi wa Chuo cha Biashara (CBE), Waziri Mkuu Majaliwa amesema lazima usimamiwe ipasavyo.
Amesema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa chuo hicho wilayani Kilolo ikiwa ni mkakati wake wa kuongeza vyuo vya biashara.
Hivyo, amewaagiza wasimamizi wa ujenzi wilayani humo kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo kikamilifu.
Amesema ameambiwa ofisa elimu Wilaya ya Kilolo ameondolewa; “hii maana yake mlitaka nikifika hapa nisibaini ‘madude’ mnayoyafanya, hata hivyo na yeye atapata onyo kali (ofisa elimu) na ajue anapaswa kusimamia miradi ya elimu kwa ukamilifu bila kumtegemea mtu,” amesema na kuongeza;
“Takukuru mkoa ingia kazini na nyie msichunguze kesi mwaka mzima na hawa nataka tujue kama wamehusika au lah. Wananchi nataka niwaambie, tutaendelea kusimamia miradi yote ya Serikali na kuchukua hatua kwa wale ambao hawatekelezi matakwa ya nchi yetu,” amesema Majaliwa.
Ameagiza halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kutumia fedha za mapato ya ndani kujenga jengo la dharura kwa ajili ya eneo la wanafunzi kupata chakula.