Mastaa Simba SC waahidi mazito, Mo avunja makundi

TULIENI. Ndivyo mastaa wa Simba walivyotoa ahadi mbele ya kikao kizito kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji’ kabla ya jioni ya leo kusepa kwenda kambini mji wa Ismailia, Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Simba inaondoka kwenda Misri kuanza safari mpya ya kimageuzi chini ya Bilionea, Mo Dewji aliyerudi na jeuri akisajili kikosi kizito na kushusha benchi la ufundi kutoka Afrika Kusini chini ya Fadlu Davids ambalo nalo pamoja na wachezaji walifanya kikao kizito na Bodi ya Wakurugenzi kuwekana sawa.

Jeshi hilo jipya la Simba, linaondoka kwa makundi mawili tu, huku asilimia 90 likiwa na makocha wote litaondoka leo mchana kwenda jijini Ismailia kuanza kambi yao hiyo ya kujiandaa na msimu mpya.

Kundi la pili litaondoka kesho Jumanne mchana kukamilisha msafara wa kikosi hicho cha kocha kijana Msauzi Fadlu aliyetua Simba akitokea Raja Casablanca ya Morocco iliyochukua mataji mawili ya huko, akiwa kocha msaidizi.

Kabla ya safari hiyo ya leo, Simba jana ilimtambulisha beki wa pembeni Valentin Nouma, huku ilikuwa inasubiriwa kumuachia hadharani beki wa kati anayemudu pia kucheza kiungo, Chamou Karaboue ikiwa ni kati ya nyota wapya walisajiliwa chini ya MO.

Mabosi wa Simba wamemaliza utata juu ya hatma ya Kocha Seleman Matola juu ya aachwe au asalie kikosini, kwani kwa sasa kiungo huyo wa zamani wa Wekundu hao ataendelea kuwa sehemu ya benchi hilo la ufundi la Fadlu atakayekuwa na wasaidizi watatu, yaani Matola, Darian Wilkens na Wayne Sandilands anayesimamia makipa, pia kuna kocha wa viungo Riedoh Berdien na Mtathimini video, Mueez Kajee.

Simba hadi jana mchana ilishatambulisha wachezaji 10 wapya, sita wa kigeni na wzawa wanne huku ikilezwa majembe mengine mawili tayari yamesaini akiwamo Karaboue aliyekuwa kitrajiwa kutambulishwa pia jana.

Wageni waliotambulishwa ni beki Valentin Nouma, winga Mzambia Joshua Mutale, mshambuliaji Mganda Steven Mukwala, viungo Charles Ahoua, Augustine Okejepha, Debora Fernandez, wazawa ni Omary Omary, Valentino Mashaka, Lameck Lawi na Abdulrazack Hamza.

Simba imelazimika kubadilika mapema ili kuepuka makosa iliyokuwa inayafanya nyuma kwa kuchelewa kambini njdio maana inaondoka mapema ikiwa fulu mziki.

Mabosi wa Simba wamefanya hivyo ikitambua ina kikosi kipya ambacho baada ya mchezo wa kirafiki wa Simba Day, itakutana na Yanga katika mechi ya kwanza ya Ngao ya Jamii. Msimu uliopita timu hizo zilikutana fainali na Simba ikashinda kwa penalti 3-1 baada ya dakika 120 kuisha kwa suluhu kabla ya Mnyama kupigwa 7-2 katika Ligi Kuu Bara.

Kutokana na hilo, Bodi ya Simba ilikutana juzi kuwekana sawa ili kuanza mwanzo mpya na nguvu, kabla ya jana Bodi hiyo chini ya Mo Dewji kukutana tena na wachezaji pamoja na benchi lote la ufundi na taarifa zinasema wachezaji wametoa ahadi ya kuwapa raha Wanasimba.

Mtendaji Mkuu, Imani Kajula ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu wa kikao cha jana akiwapa nafasi mastaa kufunguka na wao  kuahidi msimu ujao wapinzani wajiandae kwani wanaenda kambini kujifua ili warudi na moto mkali na kurejesha heshima ya Mnyama. Wachezaji na makocha pia walikuwa wakipewa ABC za kuijua Simba na falsafa hasa wageni.

Nje ya uwanja MO ameendelea na kazi ya kuunganisha timu kupitia vikao viwili vikubwa vilivyolenga kuvunja makundi na kuijenga upya Simba kama alivyoahidi wakati anarejea kuiongoza klabu hiyo.

Bilionea huyo alifanya kwanza kikao cha bodi mpya tangu alipoiunda kwa kuifumia ile ya zamani, kisha kila kitu kilienda sawa.

Baada ya kikao hicho, MO alikutana na Baraza la Ushauri lenye watu wazito wakiwemo viongozi wa juu wa zamani kama Azim Dewji, Evans Aveva, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Kassim Dewji ‘KD’, Hassan Dalali, Swedy Mkwabi na aliyekuwa mgombea nafasi ya mwenyekiti Moses Kaluwa.

Kambi ya Simba Misri itakuwa ya wiki zisizopungua tatu kabla ya kurudi mapema Agosti kuwahi Simba Day ambapo mziki mzima utatambulishwa, kisha itajiandaa na mechi za Ngao ya Jamii zitakazopigwa kati ya Agosti 8-11 na siku chache kuanza vita ya Ligi.

Related Posts