Matola aongoza msafara wa Misri, makocha wapya wabaki Dar

SIMBA imeondoka leo na wachezaji 30 kwenda nchini Misri kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa 2024/25 ikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Seleman Matola, huku makocha wapya wakiongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids wakibaki Dar.

Mbali na Fadlu, wengine wapya wanaounda benchi la ufundi la Simba ambao wote raia wa Afrika Kusini ni Darian Wilken (Kocha Msaidizi), Wayne Sandilands (Kocha wa Makipa), Riedoh Berdien (Kocha wa Viungo) na Mueez Kajee (Mtathimini Mchezo).

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema makocha hao wanatarajia kuondoka Julai 10, mwaka huu kwenda Misri kuungana na timu huku akibainisha sababu za wao kubaki kumetokana na mchakato wa kuwatafutia viza kuchukua muda mrefu kwa sababu walichelewa kufika hapa nchini.

“Kila kitu kipo tayari, hivyo wataondoka Julai 10, wakiwa na mipango madhubutu kwa ajili ya msimu ujao. Tutakuwa Misri kwa wiki tatu, hapa Tanzania tutarejea Julai 31, ili kuiwahi Simba Day itakayofanyika Agosti 3, Kisha kujiandaa na Ngao ya Jamii itakayoanza Agosti 8,” alisema.

KANOUTE, JOBE, SARR WAACHWA

Wakati wachezaji 30 wakiondoka wakiwemo wapya na wale wa zamani, Sadio Kannoute, Pa Omar Jobe, Babacar Sarr wameachwa kwenye msafara huo huku viongozi wa Simba wakiendelea na mchakato wa mazungumzo kuona namna ya kumalizana nao katika ishu ya kuvunja mikataba.

“Baada ya mazungumzo ya ndani yakifikia sehemu nzuri basi kuna taarifa nyingine itatoka, hivyo tuwe wavumilivu katika hilo ndio maana bado hatujamaliza kuwapa mikono ya kwaheri wachezaji,” alisema kiongozi huyo kuhusiana na ishu ya mastaa hao ambao msimu uliopita walikuwa sehemu ya kikosi hicho.

Pia alibainisha kwamba kipa wao, Ayoub Lakred ambaye ameongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo atajiunga na wenzake hukohuko Misri akitokea kwao Morocco.

Ikumbukwe kwamba, katika kipindi hiki cha usajili, Simba hadi leo ilikuwa imetangaza haitakuwa na wachezaji sita waliokuwepo msimu uliopita ambao ni John Bocco, Shaban Chilunda, Kennedy Juma, Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza walioachana nao, huku ikimuuza Henock Inonga. Clatous Chama mkataba wake ulipomalizika akajiunga na Yanga.

Kuhusiana na Lameck Lawi ambaye Simba ilimtangaza kuwa mchezaji wao ikimsajili kutoka Coastal Union ya Tanga, kiongozi huyo amesema suala lake wameliacha kwenye mamlaka ya soka.

Beki huyo ambaye alikuwa wa kwanza kutambulishwa ndani ya Simba kipindi hiki, kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam akiwa na kikosi cha Coastal Union kinachojiandaa kushiriki michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kesho Jumanne kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge na Azam Complex, Chamazi.

Ally alisema: “Kutokana na sintofahamu, basi kesi yake itapelekwa katika mabaraza ya soka ndio watakaoamua jambo hilo.”

Mshambuliaji wa Simba, Freddy Micheal ambaye alikuwa sehemu ya msafara wa kikosi hicho, amesema wanakwenda kujiweka fiti, ili wakirejea wawe bora katika kila mechi za Ligi Kuu pamoja na mashindano mengine.

“Maandalizi natarajia yatakuwa bora zaidi, kwani tutakwenda kupata utulivu, naamini msimu ujao tutarejea kivingine,” alisema.

Related Posts