Dar es Salaam. Siku moja baada ya Wakili Boniface Mwabukusi kuibuka na kulaani kuenguliwa kwake kuwania urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), mawakili wenzake kadhaa wameibuka kumtetea wakisema hajatendewa haki huku wakitoa wito arejeshwe miongoni mwa wagombea.
Wamesisitiza kuwa ni muhimu mawakili wapenda haki kukilinda chama chao kwa kutokubali kushiriki uchaguzi wa TLS utakaofanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma, hadi haki ya mwenzao itakapopatikana.
Wamesema kinachoendelea ndani ya chama kinaitia doa suala la utetezi wa haki na kuwa itawawia vigumu na kuwanyima uhalali wa kuhoji dhuluma kwenye uchaguzi ujao wa Serikali.
Julai 5, 2024 kamati ya rufaa za uchaguzi wa TLS ililiengua jina la Mwabukusi miongoni mwa wagombea wa urais wa chama hicho. Kuenguliwa kwa Mwabukusi kumefanya idadi ya wagombea wa nafasi hiyo kubaki watano – Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba.
Jana Julai 7, 2024, Mwabukusi alitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kupinga kuwekwa kando kwa sababu ambazo alidai hazina mashiko na kuwa atakwenda mahakamani kupinga hatua hiyo.
Sambamba na hilo, aliwataka wanachama wengine wa TLS kutoshiriki uchaguzi huo, ili kuishinikiza kamati ya rufaa ya uchaguzi iwarejeshe wagombea wote iliowaengua bila sababu za msingi.
Mwabukusi amelieleza Mwananchi leo Julai 8, 2024 kuwa tayari wamekamilisha mchakato mahakamani na wanasubiri uamuzi. “Tumekwenda mahakamani tunasubiri uamuzi halafu kesho tutaingiza nyaraka zote mahakamani,” amesema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Mawakili, Dk Eliezer Feleshi ameiambia Mwananchi kuwa ni haki ya Mwabukusi kwenda kukata rufaa mahakamani kama aliona hajatendewa haki.
“Haya mambo yapo kwenye mkondo wa uchaguzi na haki ya mwanachama. Mwanachama anapokosa haki yake ndani ya chama ana haki ya kuchukua hatua zaidi kwenye vyombo vya uamuzi,” amesema.
Kufuatia hatua hiyo, baadhi ya mawakili wamesema adhabu aliyowahi kupewa Mwabukusi ya onyo alishaitumikia, hivyo kamati ya rufaa ya uchaguzi kumuengua kwa kosa alilolitumikia ni uonevu usiokubalika.
Wameonyesha dosari ya kuenguliwa kwa wakili huyo wakisema, aliyeweka pingamizi dhidi ya Mwabukusi hakuwa na sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa TLS ya 2022, ambazo zinaeleza sifa za mtu anayepaswa kupeleka pingamizi juu ya mgombea.
Kuhusu hilo, Wakili Jebra Kambole amesema TLS inapaswa kuwa huru kimuonekano na kimatendo.
“Kama ni taasisi inayotegemewa kwenye masuala ya haki inapaswa kuwa na uchaguzi huru na haki, kama mtu ataenguliwa aenguliwe kwa msingi wa kisheria, kinyume na hapo watu waende kwenye sanduku la kura wanachama wapate uhuru wa kuamua,” amesema.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Wakili Godwin Ngwilimi akisema, TLS ni taasisi ya kitaaluma na mambo yake yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria.
Ngwilimi aliyewahi kuwania urais wa TLS mara kadhaa, amesema kifungu cha 4 cha sheria ya mawakili, inasema kazi moja wapo ya chombo hicho ni kutetea na kulinda masilahi ya mawakili wenyewe, kuishauri Serikali na wadau wengine juu ya masuala ya kisheria pamoja na kulinda jamii.
Msimamo mwingine juu ya suala hilo umetolewa na Wakili Emmanuel Chengula ambaye amesema: “Tunawataka mawakili wote kutokukubaliana na uonevu uliofanywa na kamati ya rufaa ya uchaguzi dhidi ya Mwabukusi.
“Kama kweli wagombea walikuwa na nia ya kuhakikisha TLS inalindwa kwa mujibu wa sheria, wanapaswa kukihami chama hiki kwa kukataa kuwa sehemu ya kudhulumu haki ya Mwabukusi kugombea.
“Tusiposimamia haki zetu sisi mawakili wenyewe, tuendako tutakosa wa kututetea na wa kuitetea jamii, wakati huohuo tutakosa uhalali wa kuhoji dhuluma kwenye uchaguzi za Serikali kwenye nchi yetu kwa kosa la kuhalalisha haramu,” amesema Chengula.
Kwa mtazamo huohuo, Wakili Hekima Mwasapu amesema pamoja na kamati ya rufaa kumwengua Mwabukusi ilipaswa kumpa nafasi ya kumsikiliza kabla ya kumchukulia hatua.
“Tunaona hili ni jambo la hila kumkosesha Mwabukusi sifa za kugombea wakati ana sifa za kugombea,” amesema.
Mwasapu pia amesema aliyeweka pingamizi ya Wakili Mwabukusi kuondolewa kwenye nafasi hiyo hakuwa na sifa kulingana na Kanuni za Uchaguzi wa TLS ya 2022 kifungu cha 50, ambacho kinaeleza wenye sifa ya kuweka pingamizi ni mgombea, wateule na au mawakala.
Hata aliyewahi kuwa Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala amesema kilichofanywa na kamati ya rufaa ni ukiukwaji wa utaratibu.
“Ni muhimu Wakili Mwabukusi kwenda mahakamani kwa sababu kamati imekiuka mamlaka yake na hii inaleta tafsiri mbaya kwa watu, kuwa walikuwa na nia nyingine, pia kamati hiyo inaweza kupitia uamuzi wake upya na kuurekebisha,” amesema.
Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Wakili Peter Kibatala ambaye alisema uchaguzi wa TLS ungekuwa huru na haki asingemchagua mgombea huyo lakini pia hawezi kukubaliana na yanayoendelea kwenye uchaguzi huo.
“Mawakili uchaguzi wetu unapaswa kunyooka, jambo lolote litakalofanya uchaguzi kuonekana wa konakona tunaonekana wajinga, hivyo sijakubaliana na huo uamuzi,” amesema.
Wakili Kibatala amesema atakuwa bega kwa bega na Mwabukusi kuhakikisha hakuna uchaguzi utakaofanyika kwenye mazingira yasiyo ya haki.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TLS, Francis Stolla akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu amesema Mwabukusi aliwahi kukutwa na hatia ya utovu wa maadili hivyo kupewa onyo na kutakiwa kufuata masharti ya kitaaluma.
“Kamati ya uchaguzi tuliona aliwekewa pingamizi kugombea, lakini tayari alishaitumikia adhabu, hivyo tukalitupilia mbali hilo pingamizi. Tuliona kumuadhibu mara ya pili haikuwa sahihi kisheria,” amesema.
Rais huyo wa zamani wa TLS amesema baada ya uamuzi wa kamati hiyo, mtu huyohuyo aliyekuwa amemkatia rufaa alikwenda kuweka pingamizi kwenye kamati ya rufaa ili Mwabukusi aenguliwe.
Kamati hiyo ya rufaa baada ya kupitia pingamizi hilo ilimwengua Mwabukusi kwenye orodha ya wagombea ikisema kamati ya uchaguzi ilikosea kwa kutomuondoa kwenye orodha hiyo.