Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kwa kushirikiana na Umoja wa Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), wameandaa kongamano la nishati safi, lijulikanalo kama “Energy Connect 2024”.
Kongamano hilo litafanyika Agosti 21, 2024 jijini Dar es Salaam, likiwa na lengo la kuongeza matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.
Kongamano hili linalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, sekta binafsi, wafadhili, wasomi, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na mashirika ya kimataifa.
Vilevile, litatumika kama jukwaa la kuangazia maendeleo ya hivi punde katika nishati safi na teknolojia zake, pamoja na mipango ya utekelezaji na masuluhisho ya kisasa yanayokuza uvumbuzi endelevu katika sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu, amesema dhamira ya kampuni anayoiongoza ni kukuza uendelevu na ubunifu nchini, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa umma kupitia mijadala mbalimbali.
“Tutapata suluhisho la masuala ya msingi kupitia kongamano hili. Kupitia ushirikiano huu, tunaweza kuhamasisha hatua madhubuti za matumizi ya nishati safi na Tanzania ya kijani kwa siku zijazo,” alisema Machumu.
Mwenyekiti wa ATOGS, Abdusamad Abdulrahim, alisema, “Tunafurahi kuwa wenyeji wa Energy Connect 2024 nchini Tanzania, nchi ambayo iko mstari wa mbele katika mipango ya nishati endelevu barani Afrika.
“Tukio hili litaonyesha ushirikiano kati ya nishati ya kupikia na uvumbuzi wa nishati ya kijani kwa kuonyesha ubunifu muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya mpango huu.
“Tunaamini kuwa kwa pamoja, tunaweza kupiga hatua kubwa katika kufikia mustakabali wa nishati endelevu kwa Tanzania.”
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesemi Mramba, alisema Serikali inajivunia kuunga mkono na kushirikiana na MCL na ATOGS kufanikisha Energy Connect 2024.
“Nawaomba wadau na wahusika wakuu kushiriki katika mpango huu wa nishati safi ya kupikia. Tumejipanga kuendeleza mazingira yanayohimiza ubunifu na ushirikiano katika sekta ya nishati safi. Tunaamini tukio hili litakuwa chachu ya mijadala yenye matokeo na ushirikiano utakaoleta maendeleo nchini Tanzania na kwingineko,” alisema Mramba.