Mwalimu matatani akidaiwa kumjeruhi mwanafunzi, chanzo kukataa somo la fizikia

Muleba. Jeshi la Polisi, Wilaya ya Mubela, Mkoa wa Kagera linamshikilia Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiteme, Charles Mukaluka kwa tuhuma za kumchapa viboko mwanafunzi wake, Filneth Augustine (18) hadi kumsababishia majeraha mwilini baada ya kukataa kusoma somo la fikizia.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu kwa sasa amelazwa hospitalini kwa siku nne tangu Julai 4, 2024, chanzo kikitajwa kuwa ni kichapo cha mwalimu huyo kwa kukataa kusoma somo hilo ambalo ni hiari kwa elimu ya sekondari.

Leo Jumatatu, Julai 8, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga akizungumza na Mwananchi Digital amesema tayari mwalimu huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo cha Polisi Muleba mkoani Kagera.

“Mtuhumiwa hadi sasa anashikiliwa na Polisi, kwa sababu mgonjwa bado hajaruhusiwa kutoka hospitali amelazwa, anamalizia sindano za mwisho.

“Kwa kadri madaktari watakavyoshauri kama atatolewa, basi itajulikana kama mwalimu naye atapewa dhamana au la,” amesema.

Sambamba na hilo, Dk Nyamahanga, amesema mwalimu huyo amesimamishwa kuwa mkuu wa shule, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.

Ameeleza tayari kamati ya awali ya uchunguzi wa tukio hilo iliyoundwa na Mkurugenzi wa Muleba, imeshafika shuleni na kufanya uchunguzi kujua nini kilitokea.

Awali, akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu akiwa hospitalini, mwanafunzi huyo amesema mkasa ulianza baada ya mwalimu huyo kumtaka asome somo la fizikia naye akakataa kwa kile alichodai haliwezi.

“Mkuu wa shule aliniambia kuwa si nimewahi kuongea na wewe kuhusu somo hilo? Nikamjibu ndiyo, ila siliwezi akaniambia sasa nataka leo nikuchape mpaka unisimulie,” amesema.

Baada ya mazungumzo yao hayo, Filneth amedai mwalimu huyo alimwagiza fimbo, kisha akamtaka apige magoti mbele ya wanafunzi. Wakati amepiga magoti, amedai mwalimu huyo alikuwa akiendelea na mazungumzo na wanafunzi wengine, kisha akaanza kumchapa.

Licha ya kuomba msamaha, mwanafunzi huyo amedai haikufua dafu, kwani kichapo kiliendelea huku mwalimu akimwambia atamchapa hadi afikie kumpeleka hospitali.

Baada ya kichapo hicho, Filneth amesimulia alipewa wiki moja na mwalimu wake, ili aamua ama asome somo hilo au afukuzwe shule.

“Nilijitahidi kunyanyuka, ili niende kwenye mdahalo wa shule nikafanikiwa kwa wakati huo ila nilishindwa kukaa nikalala hadi ulipomalizika na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” amesema.

Kutoka shuleni kwenye umbali wa kilomita nne hadi nyumbani, Filneth amesema alitembea kwa kuchechemea na kufika saa moja jioni.

Wingi wa fimbo hizo, kwa mujibu wa Filneth, ndio uliomsababishia maumivu makali na hivyo kulazwa hospitali hadi sasa.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Jesca Augustine (58) amesema alishangazwa kumwona mwanawe akitetemeka na mwili wake ukitokwa damu.

Kama huduma ya kwanza, amesema alikwenda kuchemsha maji ya moto kwa ajili ya kumkanda na kumwagia mwili wote, lakini kazi ilikuwa kwenye kumvua nguo kwani zilishikana na vidonda.

“Niliangalia kwenye makalio fimbo zilizopita pale ukweli nililia sana, nikachana ile siketi aliyokuwa amevaa nikamuosha na kumkanda kila eneo ila aliendelea kutetemeka na kulia huku akiugulia,” amesema Jesca.

Alipoona hali inakuwa mbaya zaidi, aliwasiliana na dada yake Filneth, kisha baadhi ya walimu ambao simu zao ziliita bila kupokelewa.

Baadaye, amesema mmoja wa walimu katika shule hiyo alifika nyumbani akitaka kumpeleka hospitali, lakini alimgomea akitaka aliyefanya kitendo hicho ndiye anayepaswa kwenda.

Saa saba usiku, mwalimu aliyehusika na tukio hilo, amedai alikwenda nyumbani hapo na walishirikiana kumpeleka hospitali.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha Kimeya alikolazwa Filneth, Dk Erasto Mosha amethibitisha kumpokea mwanafunzi huyo akiwa na majeraha mbalimbali.

“Ni kweli tulimpokea mwanafunzi huyo na mpaka sasa yuko hapa anaendelea na matibabu na uangalizi wa kina kujua afya yake. Nishauri jamii, walimu na wazazi tusiwe tunapiga watoto kiasi hiki tunawasababishia matatizo makubwa ya kiafya,” amesema.

Related Posts