Moshi. Zikiwa zimepita siku sita tangu muuguzi wa Hospitali ya KCMC, idara ya masikio, pua na koo, Lenga Masunga, kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, mwenye nyumba alikokuwa akiishi, Robert Mwakalinga, amesimulia namna alivyoamka asubuhi na kukuta mlango wa chumba alichokuwa amepanga ukiwa wazi.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani hapo leo Jumatatu Julai 8, 2024, Mwakalinga, mkazi wa Mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, amesema Jumatano, Julai 3, 2024, alipoamka asubuhi alikuta chumba cha muuguzi huyo kikiwa wazi, huku ndani kukiwa hakuna mtu. Hali hiyo ilimlazimu kukifunga chumba hicho.
Mwakalinga anasema Jumatano Julai 2, muuguzi huyo alirudi nyumbani saa mbili usiku wakati yeye alikuwa analisha mifugo yake nje, alimsalimia na akaingia ndani kama ilivyokuwa kawaida yake.
“Huyu kijana ni mpangaji wangu. Alikuja siku ya Jumanne usiku, alinikuta nikilisha kuku wangu, alinisalimia, akaingia ndani. Baadaye alikaa kama dakika tano, akatoka nje kwenda msalani, akarudi. Alipoingia ndani hakutoka tena na muda huo ilikuwa imefika saa tatu na dakika kadhaa. Nami niliingia ndani na sikutoka tena nje mpaka asubuhi,” amesema Mwakalinga.
Hata hivyo, amesimulia kuwa asubuhi alivyotoka nje, alikuta mlango wa chumba cha muuguzi huyo uko wazi.
Amesema: “Nikaita nikaona kimya, nikajiuliza imekuwaje mlango uko wazi, nilipoingia ndani, niliona mabegi yake kama yamepekuliwa na moja likiwa karibu na mlango lakini hakukuwa na mtu ndani.”
Mwenye nyumba huyo amesema tangu usiku ule walipoonana na muuguzi huyo, mpaka sasa hajui yuko wapi.
Akimwelezea muuguzi huyo, Mwakalinga amesema alikuwa sio mtu wa makundi na mara zote alikuwa akitoka kazini huingia ndani na kujifungia.
“Alikuwa sio mtu wa makundi wala kujichanganya na watu. Alikuwa akitoka kazini anaingia zake ndani na wakati mwingine akiwa ndani unaweza usijue kama yupo kama hujamwona wakati anaingia,” ameeleza.
Akimzungumzia muuguzi huyo, Mratibu wa idara ya masikio, pua na koo, Hospitali ya KCMC, Neema Masawe, amesema Julai 4, 2024, alipaswa kuwepo kazini lakini hakufika na hata alipotafutwa kupitia simu zake za mkononi hakupatikana.
“Julai 4, mwaka huu, alikuwa awe zamu ya asubuhi na kawaida yake huwa anawahi kufika hospitali mapema. Sasa ilipofika saa 1:30 asubuhi tukawa hatujamuona, tukasema labda yuko ibadani, ilipofika saa mbili asubuhi tukaona hajafika tukaanza kujiuliza kwa nini amechelewa kazini kwa kuwa si kawaida yake,” amesema Massawe.
Amesema waliamua kumtafuta anakoishi na walipofika hawakumkuta, bali walikutana na mwenye nyumba wake.
“Tukawatafuta marafiki zake wa karibu ili tujue taarifa zake, nao hawakujua wapi alipo. Baadaye tulitoa taarifa kwa uongozi wakatushauri tuendelee kumtafuta. Tuliondoka kama watano, tulimtafuta kwa saa nane bila mafanikio, tukarudi nyumbani anakoishi tukamkuta mwenye nyumba aliyetuambia alipoamka asubuhi alikuta chumba chake kiko wazi na ndani hakukuwa na mtu,” amesema Massawe.
Amesema baadaye waliamua kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Polisi Longuo na wakapatiwa RB namba LNG/RB/33/2024 na kisha kuandika maelezo.
Amesema mpaka sasa wanaendelea kumtafuta kupitia simu zao za mkononi lakini hawajafanikiwa kumpata.
Akizungumzia utendaji wake wa kazi, amesema tangu aajiriwe mwaka 2023, amekuwa ni mtu wa kujituma na mwenye upendo na kila mtu na mara kadhaa amekuwa akipongezwa kwa utendaji mzuri wa kazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.