NBC, Vodacom Tanzania waungana kufanikisha NBC Dodoma Marathon 2024

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania ili kufanikisha maandalizi ya msimu wa tano wa mbio za NBC Dodoma Marathon. Mbio hizo zenye hadhi ya kimataifa zinatarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lengo kuu la mbio hizo zinazotarajiwa kuhusisha washiriki zaidi ya 8,000 ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.

Mkuu wa Mahusiano Umma na Vyombo vya Habari wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Annette Kanora (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi hiyo na Benki ya NBC yanayolenga kufanikisha maandalizi ya msimu wa tano wa mbio za NBC Dodoma Marathon. Kulia ni Mkuu wa Mahusiano ya Umma ya Umma na Mawasiliano wa NBC, Godwin Semunyu.

Kupitia ushirikiano huo wenye thamani zaidi ya milioni 100,Vodacom Tanzania, kampuni kubwa ya mawasiliano, itakuwa mdhamini Mkuu wa mbio za kilometa 21, hatua ambayo itapeleka mbio hizo za KM 21 kufahamika “Vodacom 21Km Dodoma Marathon Race,”. Kupitia makubaliano hayo pia kampuni hiyo itakuwa mshirika wa teknolojia na mawasiliano.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika mapema leo Jumatatu katika Makao Makuu ya Vodacom Tanzania yakihusisha maofisa waaandamizi kutoka pande zote mbili huku ikishuhudiwa Mkuu wa Mahusiano ya Umma ya Umma na Mawasiliano wa NBC, Godwin Semunyu na Mkuu wa Mahusiano Umma na Vyombo vya Habari wa Vodacom, Annette Kanora wakiwakilisha taasisi zao kwenye makubaliano hayo.

Akizungumzia hatua hiyo Semunyu alisema inathibitisha jitihada na amza za pamoja  ya mashirika yote mawili katika kukuza afya ya mama na ustawi wa jumla wa jamii huku akikisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali katika kujenga jamii endelevu.

“Tunafurahi kuwakaribisha Vodacom, mshirika mashuhuri na mwenye fikra kama zetu, katika kufanikisha kusudi hili lenye nia njema kwa jamii tunayoihudumia. NBC tunaamini kwa dhati kuwa juhudi za pamoja ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazokabili jamii zetu. Kwa kutumia ujuzi na rasilimali mbalimbali, tunaweza kuongeza athari yetu na kupanua wigo wetu.

“Hivyo kwetu kama waandaaji wa mbio hizi za NBC Dodoma Marathon imekuwa ni jambo la kufurahisha kuona kuwa Vodacom ina mtazamo kama huo,” alisema.

Kwa upande wake Kanora, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya mashirika na taasisi mbalimbali hapa nchini katika kuimarisha ustawi wa jamii. “Kama Vodacom, tuna dhamira kubwa ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na kuboresha afya ya mama kote Tanzania. Kufanya kazi kwa pamoja na benki ya NBC kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon kunatuwezesha kutoa mchango wenye maana zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa Kanora, Vodacom Tanzania, kupitia miradi yake ya kijamii hususani mradi wa m-mama, imejitolea kutumia nguvu ya teknolojia ya simu kuwapatia huduma za afya kwa haraka zaidi na kwa wakati muafaka wanawake, huku ikahakikisha Watanzania wanapata huduma bora za kiafya kadili wanavyostahili.

“Kupitia ushirikiano huu, tunatumai kuchochea mabadiliko chanya katika jamii zetu, wakati tunashughulikia ajenda ya afya za kitaifa na kimataifa, huku msukumo ukiwa zaidi kwenye kukabiliana na  magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani,” alisema.

Kwa miaka mitano sasa, NBC Dodoma Marathon imekuwa ikitoa jukwaa muhimu katika kuongeza uelewa na kukusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya ya mama. Ujio wa Vodacom Tanzania kwenye mbio hizo kama mshirika wa teknolojia na mawasiliano kunalifanya tukio hilo  kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufikia malengo yake kwa viwango vipya na ukubwa uliokusudiwa huku pia zikizidi kuvutia washiriki wengi zaidi na hivyo kuzalisha athari kubwa zaidi.

Related Posts