WAKALA wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) umeelekezwa kuhakikisha mifumo yake inasomana na Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ili kuleta tija zaidi katika utekelezaji wa majukumu. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi jana Jumapili wakati alipotembelea banda la OSHA kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu Sabasaba.
Waziri Ndejembi amesema OSHA na BRELA zote ni taasisi za Serikali, hivyo katika keleta tija zinapaswa kusomana kwenye mifumo hali ambayo itapunguza mlolongo mrefu kwa wawekezaji.
“Napenda kutumia nafasi hii, kuwaelekeza OSHA kuwa mifumo yao inapaswa kusomana na BRELA, ili kurahisisha wawekezaji lakini pia kuokoa muda,” amesema.
Amesema hakuna haja ya OSHA kufika katika eneo la uwekezaji dakika za mwisho, bali inatakiwa kujua mapemba ili kuleta ufanisi katika kazi.
Ndejembi amesema iwapo taasisi hizi zitafanya kazi kwa pamoja ni wazi mafanikio ambayo Serikali inahitaji hasa katika huduma kwa wawekezaji yatafanikiwa.
Aidha, Waziri Ndejembi amewataka waajiri kujisajili OSHA, ili kuhakikisha wakala huyo anafanya ukaguzi ambao unahitajika kwenye sehemu za kazi na biashara kama sheria inavyotaka.
“Kusema kweli utendaji wa OSHA chini ya Mkurugenzi Khadija Mwenda na wasaidizi wake unaridhisha ndio maana unaona kasi ya usajili imeongezeka, endeleeni kukaza buti,” amesema.
Pia Waziri Ndejembi ameipongeza OSHA kwa kuzingatia weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, huku akiitaka isifanye uaskari na kuwa marafiki wa waajiri, hasa kwa kuwekeza kwenye elimu hasa faida ya waajiri kujisajili kwao.
Amesema OSHA imekuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za kijamii na kuchochea ukaaji wa uchumi na kuitaka iongeze nguvu zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema wameshiriki katika maonesho ya sabasaba ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za uwepo wao.
Mwenda amesema katika maonesho hayo wanatoa huduma ya usajili, kupima afya na kuonesha vifaa ambavyo wanatumia vyenye ubora wa kimataifa.
“OSHA tumeshiriki kwenye maonesho haya ya 48, ambapo tunaendelea kusajili waajiri, kupima afya kwa zaidi ya watu 300 na kuonesha vifaa vyenye ubora, hali ambayo inavutia wawekezaji,” amesema.
Aidha, kuhusu mifumo ya OSHA kusomana na BRELA, Mwenda amesema hilo lipo kwenye mikakati yao na kwamba siku chache zijazo kila kitu kitakuwa sawa.
Akizungumzia rai ya Waziri Ndejembi kuwataka watumie majadiliano zaidi katika utendaji huo, amesema hiyo ndiyo sera yao na kuahidi kuwa wataendelea.
Mtendaji mkuu huyo amesema hadi sasa wameweza kusajili sehemu za kazi 45,000, huku takribani sehemu za kazi 40,000 zikisajiliwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine Mwenda amesema katika mwaka huu wa 2024/25 OSHA itaongeza kasi ya kusajili na kukagua sehemu za kazi ikiwemo kwenye vyombo vya habari ambavyo ni wadau wa kubwa kwenye jamii.