Polisi yamsaka mzazi anayedaiwa kumuozesha mtoto kwa ng’ombe 22

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ametangaza msako mkali wa mzazi anayedaiwa kumuozesha mtoto wake wa kumzaa anayesoma darasa la nne kwa mahari ya ng’ombe 22.

Mzazi huyo anadaiwa kuchukua ng’ombe 22 kama sehemu ya mahari ya mtoto wake huyo anayesoma katika moja ya shule za msingi wilayani Uyui, ili aozeshwe.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Julai 8, 2024, Chacha amesema kwa sasa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa huo vinaendelea kumsaka mzazi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, kwani ametokomea kusikojulikana baada ya kugundua anatafutwa.

“Katika Mkoa wa Tabora hatutaruhusu watoto wadogo kuolewa au kuozeshwa kabla ya umri unaotakiwa. Pia tumepata taarifa kwamba katika shule nyingine hapa hapa Uyui kuna wanafunzi wawili wa kike walifaulu kusoma kidato cha kwanza, wakaombewa uhamisho kumbe wameozeshwa. Tunaendelea na uchunguzi pia ili watuhumiwa wote wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa (RC), amewaomba wananchi kuwalinda watoto, hususan wa kike, ili wamalize masomo yao badala ya kuwaozesha katika umri mdogo.

Kwa upande wake, Mariam Rashid, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Uyui, ameiomba Serikali kuhakikisha wanaofanya njama ya kuwaozesha watoto katika umri mdogo wanakamatwa na kupewa adhabu kali, ili iwe fundisho.

“Matendo ya ukatili kwa watoto kwenye jamii yetu yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Sisi mabinti tunaozeshwa na wazazi wetu, wengi kwa tamaa ya mali. Tunaomba Serikali na wadau wa elimu kutulinda kwa nguvu, ili tumalize elimu zetu.

“Matamanio yetu ni kumaliza elimu kama walivyo wengine kwa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Na wale watakaobainika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Mroki Fadhili, mkazi wa Uyui amesema vitendo vya kuwaozesha watoto vimekuwa vikisababisha wasichana wengi kukosa fursa ya kupata elimu inayostahili.

Ameeleza wanapoozeshwa, wasichana hao hujifungua katika umri mdogo, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

“Nawaomba wazazi wenzangu tuwalee na kuwapenda watoto wetu. Vitendo vya kuwaozesha kwenye umri mdogo vinawaharibia maisha, kwani wapo wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kuwa wanakuwa na umri mdogo,” amesema Fadhili.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, kujua jitihada za jeshi hilo katika kumsaka mzazi huyo, amesema bado wanaendelea na uchunguzi.

Related Posts