Ubovu wa barabara wakera wananchi, wachangishana kuanza ujenzi

Moshi. Changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika eneo la Kiruweni, Kata ya Mwika Kusini, Wilaya ya Moshi, imewalazimu wananchi wa eneo hilo waishio maeneo mbalimbali nchini kuchangishana fedha na kuanza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 72 kwa kiwango cha changarawe.

Eneo hilo ambalo wananchi wake wanajishughulisha na uzalishaji wa ndizi na kilimo cha mazao mbalimbali, limekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara.

Hali hii imewalazimisha kusafirisha mizigo kwa kichwa hadi sokoni, hivyo kushindwa kufikia ndoto zao za kujikwamua kiuchumi.

Chimbuko la wazo la ujenzi wa barabara lilianzia katika Usharika wa Kiruweni wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), baada ya mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa Machi na Aprili, 2024.

Mvua hizo zimesababisha barabara hizo zishindwe kupitika kwa vyombo vya usafiri, zikiwamo pikipiki.

Mtambo wa kushindilia barabara ukiendelea na kazi ya kushindilia moja ya  barabara katika kijiji cha Kiruweni, Wilaya ya Moshi,mkoani Kilimanjaro, ambazo zinajengwa kwa nguvu za wananchi. Picha na Ombeni Daniel

Akizungumza kuhusu ujenzi huo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kiruweni, Joram Mamuya amesema barabara hizo zimefikia hatua mbaya na kufanya wananchi kushindwa kutumia vyombo vya usafiri na hivyo kulazimika kubeba mazao yao kichwani kuyapeleka sokoni, huku wakitembea umbali mrefu.

“Barabara zetu zilikuwa zimefikia hatua mbaya na hazikuwa zinapitika. Mwaka huu mvua zilinyesha nyingi, barabara zimeharibika zaidi kiasi kwamba hata wananchi wanashindwa kupeleka ndizi sokoni,” amesema Mchungaji Mamuya na kuongeza:

Aidha, amesema kufuatia hali hiyo walilazimika kuwatangazia waamini na wananchi kwa ujumla kuona ni namna gani kutengeneza barabara hizo, ili kurahisisha shughuli za usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

“Tunamshukuru Mungu, wananchi wetu wanaoishi nje ya hapa waliokuja kusherekea Sikukuu ya Pasaka, ambao walikuwa ibadani siku hiyo, nao waliona changamoto hiyo na wakaamua kuchangia. Aprili 7, 2024 tulianza kuchangia kanisani na kuhamasisha kazi hiyo.

“Tuliwaomba Tarura wakafika, wakakagua barabara na kutupa ushauri namna bora ya kuzifanyia kazi. Sisi kwa pamoja tukaona tuanzie hapo. Gharama walizotupa zilikuwa kubwa, zaidi ya Sh180 milioni, lakini haikutukatisha tamaa. Tuliungana kwa pamoja kama jamii na kuanza kazi hii,” amesema mchungaji huyo.

Mtambo wa kumwagilia maji barabara ukiendelea na kazi hiyo katika moja ya  barabara katika kijiji cha Kiruweni, Wilaya ya Moshi,mkoani Kilimanjaro, ambazo zinajengwa kwa nguvu za wananchi. Picha na Ombeni Daniel

Wakizungumza baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, wamesema ujenzi wa barabara hizo utawawezesha kusafirisha mizigo yao kwa urahisi kutoka nyumbani hadi sokoni na kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.

John Tarimo, amesema barabara hizo walizoea kuzitengeneza kwa majembe ya mkono kupitia msaragambo wa kijiji, lakini kwa sasa hilo lilishindikana kutokana na mvua ambazo ziliharibu zaidi barabara hizo.

Anasema baadhi zilijifunga na nyingine kuwa na mashimo makubwa ambayo yalifanya zisipitike.

“Barabara zetu tumekuwa tukizitengeneza kwa majembe ya mikono na mbaya zaidi kwa sasa kijijini huku hakuna vijana, ni wazee ambao hawawezi kutoka msaragambo kutengeneza barabara, hali iliyosababisha barabara kuharibika na kutopitika kabisa. Hii imechangiwa zaidi na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu,” amesema.

Moja ya barabara zinazoendelea kutengenezwa katika kijiji cha Kiruweni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Omben Daniel

Tarimo amesema Aprili walivyokwenda kijijini huko, barabara zilikuwa hazipitiki. Kupitia uongozi wa kanisa, wananchi wa eneo hili walijichangisha na kuwashirikisha Wana-Kiruweni wanaoishi maeneo mbalimbali nchini. “Tukashirikishana changamoto hiyo na hivyo tukakubaliana kuchangishana, ili kufungua barabara zote za kijiji hiki ambazo mtandao wake ni kilometa 72,” amesema Tarimo.

Amesema asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji hicho ni wakulima, wanahitaji mazao yao yasafirishwe kupeleka sokoni, hali iliyowafanya wengi kuyabeba kichwani kufikia soko kutokana na ubovu wa barabara.

Amesema kutokana na Serikali kukabiliwa na mambo mengi, anatoa wito kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kuanza kuchukua hatua ya kutatua changamoto zinazowakabili watu waishio vijijini.

“Tusisubiri kila kitu kifanywe na Serikali. Pale wanapoweza kufanya waunganishe nguvu kama jamii na kufanya jambo, wajitokeze na kufanya. Watu wanapotoka vijijini na kwenda mijini, wakifanikiwa wasisahau nyumbani. Warudi nyumbani kuboresha mazingira ya kwao,” amesisitiza Tarimo.

Shicha Mmbando, mkazi wa kijiji hicho, amesema wameamua kutoa sehemu ya mashamba yao na nguvu kazi, ili kuhakikisha miundombinu ya barabara inapitika kwa urahisi wakati wote wa mvua na kiangazi.

“Barabara zilikuwa ni changamoto. Tunatembea zaidi ya kilometa 10 na mizigo kichwani tukitoa mazao shambani maeneo ya Riata na Holili. Tunapeleka mizigo kichwani kwa sababu magari hayawezi kupita, tunashukuru zikikamilika sasa maisha yatakuwa rahisi,” amesema.

Related Posts