UWANJA WA NDEGE WA IRINGA UANZE KAZI AGOSTI MOSI – MAJALIWA

 

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 23 kwa Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, taasisi zinazosimamia sekta ya anga na uongozi wa mkoa wa Iringa kutatua vikwazo vilivyopo ili uwanja wa ndege wa Iringa uanze kutumika ifikapo Agosti mosi, mwaka huu. 

 

Ametoa agizo hilo leo (Julai 8, 2024) wakati akizungumza na viongozi na wananchi mbalimbali waliokuwepo uwanjani hapo mara baada ya kukagua ujenzi wa uwanja huo. Gharama za ujenzi wa uwanja huo ni sh. bilioni 63.7 na gharama za usimamizi ni sh. bilioni 1.1.

 

“Nimesema Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, TAA, ATCL, Mamlaka ya Hali ya Hewa, TANROADS na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa wakae, wafanye vikao na kuondoa vikwazo kabla ya tarehe 30 Julai ili ifikapo tarehe 1 Agosti, 2024 uwanja huu uanze kufanya kazi,” amesema. 

 

Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba juhudi za Rais Dkt. Samia za kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour zimeanza kuzaa matunda kwa idadi ya watalii wanaokuja nchini inazidi kuongezeka. 

 

“Idadi ya watalii wanaokuja nchini ni kubwa, wengi wanaenda Serengeti. Tunataka waje huku kanda ya Kusini, na kwa kuanzia, barabara ya kutoka Iringa Mjini hadi kwenye geti la Hifadhi ya Ruaha itajengwa na Benki ya Dunia kwa kiwango cha lami.”

 

Amesema ujenzi wa uwanja wa Iringa umefikia asilimia 93 na uwanja huo ni wa viwango vya kimataifa. “Tukikamilisha uwanja wa ndege na barabara ya lami, ni wazi kuwa pato la mkoa wa Iringa litaongezeka.”

 

“Wana-Iringa jipangeni kwa fursa zilizopo, kule mbugani wanahitaji kuwe na mahoteli, wanahitaji vyakula zaidi na magari ya utalii ili yapeleke watalii kwa urahisi zaidi.”

 

Amemwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba aunde timu ya kutangaza vitutio vya mkoa wa Iringa ikiwemo kuipaisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Related Posts