Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewaomba wafanyabiashara wa eneo la Soko la Simu 2000 kufungua maduka na vibanda vyao vya biashara ili kuruhusu mazungumzo kati yake na wafanyabiashara hao aliyopanga yafanyike Jumamosi tarehe 13 Julai mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Chalamila ametoa kauli hiyo leo Jumatatu alipofika katika eneo hilo la Simu 2000 na kuzungumza na wafanyabiashara hao ambao wamegoma kufungua maduka yao na kufunga barabara kushinikiza manispaa ya Ubungo isikabidhi eneo hilo kwa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART).
Wafanyabiashara hao maarufu kama wamachinga wameandamana huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali, wakilalamikia uongozi wa Ubungo kukabidhi eneo hilo DART ili wajenge karakana ya mabasi yao.
Akizungumza nao, Chalamila amesema; “Niwaombe muendelee na biashara, nivumiulie mpaka Jumamosi ili mambo yaende kwa uwazi kwa sababu na mimi nilikuwa nasikiasikia tu.”
Aidha, amekiri wafanyabiashara hao hawakushirikishwa katika mchakato huo wa kutwaa eneo hilo jambo ambalo amesema si sahihi.
Awali wafanyabiashara hao walimtimua Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko kwa madai kuwa wamekosa imani naye kwa sababu ameshindwa kutatua changamoto zao.
Walidai kuwa kuna taarifa zimetolewa na Meya wa Manispaa hiyo kuhusu uamuzi huo wa kukabidhi eneo hilo la Simu 2000 kwa DART ilihali wao hawakushirikishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madai hayo, mkuu huyo wa wilaya amekana madai ya manispaa hiyo kukabidhi eneo hilo la Simu2000 kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kwa ajili ya ujenzi wa karakana na badala yake amesema kumekuwa na vuguvugu la kisiasa ambalo linalenga kuitisha serikali ili iache mambo yaende holela.
Bomboko amesema mbali na mdai hayo, pia kuna taarifa kuwa raia mmoja wa kigeni kutoka China amekabidhiwa eneo hilo taaria ambazo amedai zote si sahihi.