Wafanyabiashara Simu200 wamfukuza DC Ubungo

Dar es Salaam. Katika mgomo wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga eneo la Soko la Simu2000, Ubungo jijini Dar es Salaam, wamedai wamekosa imani na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko katika kushughulikia changamoto zao.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kile walichoeleza kuwa licha ya kumlalamikia mara kadhaa kuhusu changamoto zao, ameishia kuwaahidi kwenda kuzifanyia kazi bila kuwapo utekelezaji.

Wafanyabiashara hao wamegoma kufungua biashara zao na kuandamana leo Jumatatu Julai 8, 2024 wakishinikiza Manispaa ya Ubungo ifute uamuzi wake wa kukabidhi eneo hilo kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Manispaa hiyo imetangaza kulikabidhi eneo hilo kwa Dart, Julai 4, 2024 baada ya kikao cha baraza la madiwani na kueleza kikao hicho kimeridhia Dart ijenge karakana yake.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa kamati ndogo ya maboresho ya soko hilo, Mussa Ndile amesema walikubali kuhama kutoka barabarani kwenda sokoni hapo bila tatizo.

Hatua yao ya kukubali kuhama barabarani ilitokana na kile alichoeleza waliahidiwa eneo la Simu2000 linaendelea kutumiwa nao wakati wote.

Ameeleza kilichowapa imani zaidi ni hatua ya Serikali kutumia fedha takriban Sh300 milioni kuboresha eneo hilo, lakini sasa wanasikia taarifa ya kukabidhiwa kwa Dart.

Hofu waliyonayo, amesema ni pengine wakajikuta wanarudia utaratibu wa kuhamishwahamishwa kama ilivyokuwa kabla ya mpango wa kuwapanga wamachinga.

Rose Ndosi, mfanyabiashara katika soko hilo amesema wamekopa fedha nyingi kupitia Vicoba na taasisi mbalimbali za fedha, lakini hawaoni matarajio ya kulipa madeni iwapo Dart itakabidhiwa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Rose, tumaini lao ni Waziri Mkuu, Waziri wa Biashara na Viwanda au Rais Samia Suluhu Hassan.

Magari ya vikosi vya ulinzi na usalama yameanza kuwasili katika maandamano hayo yaliyoanza saa 1:00 asubuhi.

Mbali na kufunga biashara zao, pia wameweka vizuizi katika barabara kuelekea Sinza na kuzuia magari kuingia na kutoka katika Kituo cha Daladala cha Simu2000.

Nyimbo za ‘hatutaki karakana tunataka soko letu’ ndizo zilizokuwa zikisikika zikiimbwa na waandamanaji katika eneo hilo.

Mgomo na maandamano hayo uliambatana na mabango yaliyochapishwa jumbe mbalimbali, ikiwemo ‘hatutaki karakana Simu2000 Mama Samia njoo ututetee.’

Saa 3:26 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bomboko alifika eneo hilo na polisi, lakini wafanyabiashara hao walimtaka aondoke.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts