Wanariadha waiangukia Serikali maandalizi duni, vifaa

KUKOSEKANA kwa maandalizi mazuri ikiwemo kambi na vifaa bora vya mazoezi kumewaibua baadhi ya wanariadha wa Tanzania ambao wameishauri Serikali kuingilia kati na kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi.

Baadhi ya wanariadha hao wakizungumza baada ya kushiriki mbio za Lake Victoria Marathon zilizofanyika juzi jijini Mwanza, wamesema Tanzania ina wanariadha wengi lakini wanakosa maandalizi mazuri ikiwamo kambi huku wengine wakikosa mlo kamili wakati wa maandalizi.

Mwanariadha, Tunu Andrea akizungumza baada ya kuibuka mshindi wa pili wa mbio za kilomita 21 wasichana, alisema Tanzania inao wanariadha wengi lakini wanakatishwa tamaa na malipo kiduchu kwenye mbio mbalimbali zinazoandaliwa nchini.

“Tunaomba Serikali itusapoti wanariadha kwa kuweka kambi kwa ajili ya mazoezi, malazi na chakula kwa sababu mchezo huu unahitaji nguvu na wanariadha wengi hawapati milo mizuri kwahiyo wakazane kutusaidia kwa sababu changamoto ni nyingi na zinakatisha tamaa,” alisema Tunu.

Kwa upande wake, Shing’ade Giniki aliyeshinda kilomita 21 wavulana katika mbio hizo, alisema maandalizi mazuri ikiwemo kambi, makocha bora na nidhamu ndiyo siri ya wanariadha kufanya vizuri, jambo ambalo limemsaidia kung’ara baada ya mwaka jana kumaliza katika nafasi ya pili.

“Siri ya ushindi ni mazoezi, mbio ni ajira kwa wanariadha wengi lakini kwenye riadha bado wachezaji tunapata changamoto nyingi ikiwemo kupata vifaa bora vya kufanyia maandalizi. Mashindano yanahitaji mazoezi na maandalizi mazuri na kuwa nidhamu ya kumsikiliza kocha,” alisema Giniki.

Mratibu wa Lake Victoria Marathon ambazo zinafanyika kwa msimu wa nne zikishirikisha wanariadha zaidi ya 1,000 nchini, Hilda Vigo alisema Serikali inapaswa kuboresha na kuwawezesha wanariadha mahitaji muhimu ya mchezo huo ili wafanye vizuri na kutoa ushindani kwa washiriki kutoka nje ya nchi.

Related Posts